Na Ahmad Mmow, Lindi.
Balozi wa Indonesia nchini Tanzania, Profesa Ratlan Pardede ameahidi kutafuta soko la madini ya aina ya jasi nchini Indonesia ili kukabilianana changamoto ya kutokuwepo kwa masoko ya uhakika ya madini hayo.
Profesa Pardede alitoa ahadi hiyo jana katika kijiji cha Kiranjeranje, wilayani Kilwa alipotembelea eneo linalo tumika kupakia na kusafirisha jasi inayotoka migodini.
Profesa Pardede ambae aliahidi hio baada ya kusikia maelezo ya katibu wa wachimbaji wadogo wa jasi katika wilaya ya Kilwa, Elias Kabwebwe, alisema baada ya kusikia maelezo na changamoto zilizoelezwa atatafuta masoko ya madini hayo nchini Indonesia ili wachimbaji wanufaike na kazi wanayofanya.
Licha ya ahadi hiyo, pia Profesa Pardede aliahidi atazungumza na kampuni zinazotengeneza bidhaa zinazotokanana jasi nchini Indonesia kuja kujenga viwanda vinavyotengeneza bidhaa zinazotokanana madini hayo.
Awali katibu wa umoja wa wachimbaji wadogo wa jasi wilayani Kilwa, Elias Kabwebwe alisema licha ya jasi inayopatikana wilayani humo kuwa bora kuliko inayopatikana katika nchi nyingine zote zilizopo barani Afrika, lakini miongoni mwa changamoto kubwa ni soko la uhakika.
Kabwebwe pia alisema litakuwa jambo jema iwapo kutajengwa viwanda vya kutengeneza bidhaa zinazotokanana madini hayo wilayani Kilwa ili kuyaongezea thamani na kuzalisha ajira kwa wananchi. Huku akiitaja changamoto nyingine kuwa ni mitaji midogo. Hali inayosababisha watumie vifaa duni vya kuchimbia.
Licha ya kutembelea eneo hilo katika wilaya hiyo ya Kilwa, balozi Profesa Pardede alitembelea vivutio vya utalii vya mambo ya kale katika eneo la Kilwa Kisiwani. Ambapo pia alifanya utalii wa baharini.


No comments:
Post a Comment