Mtu huyo ambaye mamlaka za Kenya zimemtambulisha zikidai ni raia wa Tanzania, ni miongoni mwa watu wawili waliokamatwa na kikosi maalum katika eneo la Likoni, Mombasa wakiwa kwenye harakati za kupanga mashambulizi katika maeneo ya bandari na maduka makubwa.
Balozi wa Tanzania nchini Kenya, Dk John Simbachawene amesema leo Ijumaa Agosti 27,2021 kuwa wanafahamu taarifa za kukamatwa kwa watu hao lakini, bado wanafuatilia ili kufahamu kama kweli ni Mtanzania.
Amesema tangu kutokea kwa tukio hilo taarifa mbalimbali zimekuwa zikisikika hivyo, wanahitaji umakini zaidi kupata uthibitisho ndipo watoe taarifa. Pia, amesema kuwa wanaendelea kufuatilia kwa karibu kutafuta uthibitisho wa madai kuwa ni Mtanzania kwa kuwa, wanasikia akitajwa pia kuwa raia wa nchi nyingine.
"Ni kweli kuna hilo tukio la watuhumiwa hao kukamatwa na mmoja kudaiwa kuwa ni Mtanzania. Lakini, kuna taarifa nyingi sana zinasikika hivyo tunafuatilia kujua kipi sahihi. Tutatoa taarifa baada ya kujiridhisha," amesema Balozi Simbachawene.
Katika tukio hilo watu wawili walikamatwa na maofisa Kikosi Maalum na Kitengo cha Polisi cha Kupambana na Ugaidi (ATPU) walipokuwa kwenye gari aina ya Toyota Probox yenye namba za usajili KCE 695U kabla ya kutekeleza shambulio hilo.
Maofisa hao waliwazingira na kuwavamia wawili hao walipokuwa wakizozana na maofisa wa kivuko hicho kuhusu malipo ya kuvusha gari lao.
Wakati wa ukamataji huo, watuhumiwa hao walidaiwa kukutwa na bunduki mbili za AK-47, simu za mkononi pamoja na risasi 150. Mpaka sasa mamlaka za Kenya zimegoma kutaja majina ya watuhumiwa hao kwa kile kinachodaiwa kutaharibu ushahidi.

No comments:
Post a Comment