Kundi la Wanamgambo wa Taliban limewatolea wito viongozi wa dini ya Kiislamu nchini Afghanistan kuhimiza amani wakati wa sala ya Ijumaa baadaye leo ambayo ni ya kwanza tangu wapiganaji wake walipochukua udhibiti wa taifa hilo.
Taliban imewataka maimamu kutumia mahubiri ya ibada ya leo kuhimiza watu kulinda amani na utulivu pamoja na kuwashawishi kutoikimbia nchi hiyo baada ya kuongezeka kwa wasiwasi kwamba utawala wa kundi hilo utakuwa wa kikatili.
Wito wa Taliban unakuja wakati maandamano ya kulipinga kundi hilo yakisambaa kwenye miji mingi nchini Afghanistan ikiwemo mji mkuu, Kabul na kuna ripoti za watu kuuwawa.
Mashuhuda wamesema watu kadhaa wameuwawa baada ya wapiganaji wa Taliban kufyetua risasi za moto kwenye mkusanyiko mkubwa katika mji wa mashariki wa Asadabad jana Alhamisi.
Ingawa kwa jumla hali ni ya utulivu nchini Afghanistan lakini kumekuwa na ripoti za wapiganaji wa Taliban kutumia nguvu kuwadhibiti waandamanaji.
No comments:
Post a Comment