Hissène Habré, mtawala wa zamani wa Chad ameaga dunia akiwa na umri wa miaka 79 wakati anatumikia kifungo cha maisha kwa uhalifu dhidi ya binadamu.
Alikuwa akipata matibabu baada ya kupata maambukizi ya virusi vya corona, ripoti zimesema.
Habré alipatikana na hatia mwaka 2016 baada ya uhalifu uliofanywa wakati akiwa rais tangu mwaka 1982 hadi 1990.
Hatia hiyo ilikuwa matokeo ya kesi ya kihistoria nchini Senegal.
Ilikuwa ni mara ya kwanza kwa mahakama inayoungwa mkono na Umoja wa Afrika kumshtaki mtawala wa zamani wa ukiukwaji wa haki za binadamu.
Habré alishtakiwa kwa kuhusika na ubakaji, utumwa wa kingono na kuamuru mauaji wakati akiwa madarakani. Alikana mashtaka dhidi yake.
Wakati wa kesi hiyo, manusura walisimulia maelezo ya kutisha ya mateso yaliyofanywa na polisi wa siri wa Habré.
Mnamo 1990, aliangushwa na waasi, mwishowe akatafuta kimbilio nchini Senegal. Miongo miwili baadaye, mahakama nchini Chad ilimhukumu kifo bila kuwapo mahakamani kwa makosa ya uhalifu dhidi ya ubinadamu.
Akizungumzia kifo cha Habré, Reed Brody, ambaye alikuwa amefanya kampeni kwa rais wa zamani kushtakiwa, alisema Habre alikuwa mmoja wa madikteta wasio na huruma ulimwenguni, mtu aliyewaua watu wake mwenyewe".

No comments:
Post a Comment