Kamanda wa Polisi Mkoa wa Songwe, Janeth Magomi amesema ajali hiyo ilitokea katika barabara ya Tunduma- Mbeya katika kijiji cha Hanseketwa saa 11:45 alfajiri.
Amesema wafanyakazi wanne walikuwa wa Mkoa wa Mbeya na mmoja wa Tunduma mkoani Songwe na walikuwa katika doria na walihisi gari moja kupakia mzigo wa magendo na kuamua kulifukuza.
Akitoa salamu za pole mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Juma Homera amesema watumishi hao walikuwa vitani wakilitumikia Taifa na kuwaomba ndugu, jamaa na marafiki kuwa wapole na kuvuta subira katika kipindi hiki kigumu.
"Hawa walikuwa ni wapigania nchi ili ipate vituo vya afya, barabara, elimu na maendeleo ya nchi kwa ujumla, niwaombe ndugu, jamaa na marafiki kuwa na subira katika kipindi hiki na Serikali itakuwa pamoja, " amesema Homera.
Mkurugenzi wa utawala wa Mamlaka ya mapato nchini (TRA), Michael John amesema ni pigo kuwapoteza watumishi hao ambao walikuwa wamejitolea maisha yao kuitumikia nchi.
"Walikuwa wamejitoa kwa nguvu zao kuitumikia Taifa ni pigo kubwa katika mamlaka na Serikali kwa ujumla, tunawaombea wapumzike kwa amani, " amesema John.
Askofu wa Kanisa la EAGT Mkoa wa Mbeya, Agustino Mwakatage amesema lazima muda wote watu wajikite kwa Mungu kwani maisha ya dunia ni mafupi na muda wowote lazima kujiandaa.
Katibu wa Sheikh wa Mkoa wa Mbeya, Abas Juma akitoa salamu kwa niaba ya Baraza Kuu la Waislamu mkoani humo (Bakwata) amesema kiimani mtu anayekufa wakati wa kazi anakuwa bora, huenda marehemu hao wakapokelewa vyema na Mungu.

No comments:
Post a Comment