Makumi ya miili imepatikana katika mto unaoashiria mpaka kati ya Ethiopia na Sudan, wakaazi wa upande wa Sudan wameripoti.
Baadhi ya miili ilikuwa na majeraha ya risasi na mikono kufungwa.
Mto Setit unaofahamika Ethiopia kama Tekeze unapitia eneo la Tigray linalokumbwa na mzozo kaskazini mwa Ethiopia ambako vikosi vya serikali na washirika wake wanapigana na waasi wa Tigray.
Mhudumu wa afya ambaye alitorokea nchini Sudan ameiambia shirika la Habari la Reuters kwamba alikizika miili 10 katika wiki moja iliyopita. Anasema miili mingine 28 iliopolewa, ikiwemo saba siku ya Jumatatu.
Shirika la habari la AP limemnukuu afisa wa Sudan akisema mamlaka katika mkoa wa Kassala ilikuwa imepata miili 50, inayodaiwa kuwa ya watu wanaotoroka vita.
Serikali ya Ethiopia haijatoa tamko rasmi kuhusiana na miili hiyo. Akaunti ya Twitter inayoendeshwa na serikali hapo jana iilisema kampeini ya "propaganda" kuhusu "mauaji feki" huko Humera – ambako mto Tekeze unapitia- "imefufuliwa tena kwa kutumia picha za uwongo zinazoonesha picha za kikatili”.
Mapigano katika eneo la Tigray yalianza mwezi Novemba kati ya utawala wa jimbo hilo Tigray People's Liberation Front (TPLF), na serikali ya muungano.
Vita hivyo vya miezi minane vimesababisha mzozo mkubwa wa kibinadamu huku maelfu ya watu wakikabiliwa ha hali ya njaa.

No comments:
Post a Comment