Na Baraka Messa
Mkuu wa Wilaya ya Ileje Anna Gidarya amewataka wasichana wilayani Ileje kujiunga na jeshi la akiba la Mgambo ili kuboresha maadili malezi na kujenga jamii iliyo bora.
Alisema hayo juzi katika ufunguzi wa mafunzo ya jeshi la akiba Mgambo katika kata ya Ngulugulu Tarafa ya Bundari wilayani Ileje.
Alisema mafunzo ya Mgambo ambayo hufanyika nchini kote kwa awamu tofauti tofauti husaidia vijana kuwa wazalendo, wachapakazi na uwajibikaji kwa kiasi kikubwa.
Alisema mafunzo hayo ni kwa ajili ya vijana wote wa kiume na upande wa kike, hivyo kuwataka wazazi kuwahamasisha vijana wao wa kike kujiunga na jeshi hilo la akiba.
"Wazazi wahamasisheni watoto wenu wa kike kujiunga na fursa hii muhimu, watoto wa kike wakipata mafunzo yatawasaidia kujenga jamii iliyo bora kutokana na malezi watakayoyapata kwenye mafunzo" alisema Gidarya.
Gidarya alishangazwa baada ya kukututa kati ya vijana 133 ambao tayari wameanza mafunzo hakuna kijana wa kike hata mmoja.
"Kwenye jamii zetu kuna changamoto nyingi zinazo tuhusu wanawake ambazo zinahitaji kutatuliwa , hivyo wakipata mafunzo hawa watatusaidia kuzitatua , Haya mafunzo sio adhabu hii ni sehemu ya malezi kwa vijana wetu wa kike na kiume ambayo yana manufaa kwao na kwa Taifa" aliongeza Gidarya.
Afisa Tarafa ya Bundari Nickson Mwashitete alisema mara ya mwisho mafunzo kufanyika katika kata ya Ngulugulu kuwa ilikuwa mwaka 1996 hivyo kuwataka wazazi kuwahamasisha vijana kupata mafunzo.
Alisema vijana waliojiandikisha kupata mafunzo ni 375 lakini mpaka Sasa walioripoti na kuanza mafunzo ni 133 tu.

No comments:
Post a Comment