Search This Blog

Thursday, August 12, 2021

Maziwa ya mama huepusha vifo vya watoto


Na Baraka Messa Songwe.

MKURUGENZI mtendaji Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania Dk Germana Leyna amesema unyonyeshaji mzuri wa maziwa ya mama ndani ya miezi sita ya mwanzo huepusha vifo  mbalimbali vya watoto ambavyo hutokea kwa wingi Duniani.

Alisema hayo hivi karibuni katika maazimisho ya wiki ya unyonyeshaji yaliyofanyika wilayani Mbozi  Mkoani Songwe, huku akiwataka watanzania kuzingatia unyonyeshaji katika miezi sita ya mwanzo baada ya mtoto kuzaliwa.

Alisema utafiti unaonyesha kuwa takribani  vifo 823,000 vya watoto na 20,000 vya wanawake vinavyotokea wakati wa kujifungua duniani kila mwaka vinaweza kuzuiwa kutokana na unyonyeshaji .

Aliongeza kuwa maziwa ya mama yamethibitika kuwa na virutubisho vinavyomtosheleza mtoto kwa miezi sita ya mwanzo endapo unyonyeshaji utafanyika kwa usahihi.

“Faida ya kumnyonyesha mtoto maziwa pekee ya mama katika miezi sita ya mwanzo ni nyingi lakini muhimu zaidi ni kupambana na magonjwa ya kuhara ambapo watoto wasionyonyeshwa maziwa ya mama wana hatari ya kuharisha mara 25 zaidi ya wanaonyonya “ alisema Leyna.

Kwa upande wake Mganga mkuu wa mkoa wa Songwe Hamad Nyembea alisema kuwa pamoja na mkoa wa Songwe kuwa miongoni mwa mikoa mitatu nchini kwa uzalishaji wa chakula kingi lakini bado unakumbwa na changamoto ya utapaia mlo na udumavu na kuwa miongoni mwa mikoa mitano iliyo kithiri kwa udumavu.

Alisema kwa upande wa unyonyeshaji  Mkoa wa Songwe wamekuwa wakitoa elimu katika vituo vya afya na zahanati na kufikia asilimia 60 ya unyonyeshaji tofauti miaka ya nyuma.

Mkuu wa Wilaya ya Mbozi Cosmas Nsenye Alisema maziwa ya mama ni chakula bora kwa mtoto , kwani humpatia virutubisho vyote na maji anayohitaji  kwa ukuaji katika miezi sita ya mwanzo ikiwa ni pamoja na maziwa  mazito ya njano ambayo huitwa kolostram yanayotoka siku chache za mwanzo husaidia kumkinga mtoto dhidi ya maradhi mbalimbali.

Alisema takwimu zinaonyeshakuwa  asilimia 55.5 watoto huanza kunyonya baada ya saa moja kuzaliwa , asilimia 58 watoto hunyonya maziwa pekee ya mama kwa muda wa miezi sita ya mwanzo, asilimia 52 watoto hunyonya kwa muda wa mwaka mmoja baada ya kuzaliwa.

Aliongeza kuwa kwa upande wa watoto wanaonyonya mpaka kufikisha miaka miwili baada ya kuzaliwa kuwa ni asilimia 43 tu, wanaoanzishiwa  vyakula vya ziada katika umri sahihihi kuwa ni asilimia 35 na wanaopata mchanganyiko sahihi ya kukidhi mahitaji ya mwili wa mtoto kuwa ni asilimia 30.

“unyonyeshaji wa mtoto kwa ndani ya miezi sita maziwa ya mama pekee huimalisha afya ya mama na mtoto , lakini pia ndio msingi wa maendeleo ya nchi kwa kuwa huweza kuzuia aina zote za utapia Mlo” alisema Nsenye.

 



No comments:

Post a Comment

Punguza kilo tano kwa siku saba

  NI watu wachache wanaopenda kunenepa, wengi wanapenda miili ya wastani kwa kuwa  unene si mzuri. Ukiwa mnene si tu kwamba unakaribisha m...