Na John Walter-Hanang.
Mkuu wa wilaya ya Hanang mkoani Manyara Janeth Mayanja, amewataka maafisa kilimo kuwatembelea Wakulima wa kilimo cha Shayiri na ngano mashambani na kutoa ushauri na maelekezo ya kulima kitaalamu ili kupata tija kwenye kilimo chao.
Akizungumza katika sherehe za uzinduzi wa msimu wa Mavuno kwa zao la Shayiri katika Kata ya Nangwa Wilayani humo iliyoandaliwa na kampuni ya YARA, Mayanja amesema maafisa hao wakifanya Kazi zao kikamilifu kwa kuwa karibu na wakulima wakati wa msimu wa kilimo unapoanza itasaidia wakulima kuacha kilimo cha mazoea hali itakayowaletea tija.
Amewataka maafisa Ugani kuwafuata Wakulima mashambani na kutatua changamoto zote za Kilimo na kuwashauri na kupata takwimu na taarifa zote za Wakulima wanalima mazao gani na Hekari ngapi na maendeleo yote kwa ujumla.
Amesema ili kupata mafanikio zaidi ni vyema wakulima wakawa na kumbukumbu sahihi kuanzia wanapoanza kilimo hadi mavuno ili mwisho kutambua kila hekari yamepatikana mazao kiasi gani na shilingi ngapi pamoja na kufungua akaunti kwenye mabenki yaliyomo nchini kuhifadhi fedha zilizopatikana.
Amesema wilaya ya Hanang uchumi wao mkubwa unatokana na kilimo na ufugaji ambapo wakulima ni asilimia 80 hivyo amewaomba wadau wa maendeleo katika sekta ya kilimo kujitokeza kuwasaidia wakulima na wilaya kwa ujumla katika kuhakikisha kilimo kinafanywa kwa tija na uzalishaji kuongezeka ili kuongeza mapato ya serikali na kwao pia.
Ameipongeza kampuni ya YARA kwa uhamasishaji ambao wanaufanya kwa wakulima Kwani imewasaidia wananchi kupanda kwa kutumia mbolea na kuongeza wingi wa mavuno.
Kwa upande wake bwana shamba wa kampuni ya Uagizaji na usambazaji wa mbolea Tanzania (YARA) Novatus Alala amesema miongoni mwa malengo yao ni kuilisha na kuilinda dunia, kuhamasisha matumizi sahihi ya mbolea kwa wakulima kupitia mashamba darasa,semina za wakulima na kuwatembelea kwenye mashamba yao ili kuongeza tija kwa wakulima.
Aidha amesema YARA hubuni mbinu sahihi ya kilimo kwa kutumia njia za kisasa na kuwapatia wakulima uwezekano wa kupata mshauri popote pale walipo kwa njia ya simu na mitandao ya kijamii.
Kwa upande wake kaimu Afisa Kilimo Wilaya ya Hanang Vicent Mshana ameeleza katika msimu huu wa mavuno wanatarajia kuvuna zaidi ya Tani 1000 kutokana na wakulima wengi kulima kwa kuzingatia teknolojia ya kisasa ya kutumia mbolea.
Mkulima wa Shayiri aliyetumia mbolea ya YARA Bwana Peter Kepa anasema baada ya kupata ushauri kutoka kwa bwana shamba wa Yara anao uhakika wa kuvuna gunia kuanzia 12 hadi 15 kwa hekari moja tofauti na awali kabla ya kuanza kutumia mbolea ambapo alikuwa akipata gunia zisizopungua tano kwa hekari.
No comments:
Post a Comment