Vijana wanaopata mafunzo ya jeshi la akiba katika kijiji cha Lositete wameaswa kuwa na nidhamu zuri kwa wakufunzi katika kipindi chote cha mafunzo. Sifa kubwa ya askari ni nidhamu, ili tuweze kutimiza malengo na kukamilisha vipindi vyote vya mafunzo tunapaswa kujituma kwa kuzingatia muda.
Hayo yamesemwa katika uzinduzi wa mafunzo ya jeshi la akiba katika kijiji cha Lositete na Mkuu wa wilaya ya Karatu Mh. Abbas Kayanda. Amesema ili kufanya mafunzo haya kuna kibali cha ngazi ya taifa na kibali kutoka mkoani ili kuridhia kufanyika kwa mafunzo ya jeshi la akiba. Ameongeza kusema tunapaswa kumshukuru Rais wa jamhuri ya muungano wa Tanzania Mh. Samia Suluhu Hasani kwa kibali cha kufanya mafunzo haya ya jeshi akiba.
Amesema mafunzo ya mwisho ya askari wa jeshi la akiba yalifanyika mwaka 2003 na mfunzo haya yamezingatia uhitaji mkubwa wa kijiji cha lositete ambayo yanahusisha vijana 85 kati yao wasichana ni 7 na wavulana ni 78. Mafunzo ya jeshi la akiba yanafanyika kwa mujibu wa sheria ili kuendelea kutunza hali ya ulinzi na usalama wa taifa, rasilimali za kijiji, na ulinzi wa makazi ya wananchi. Amesema kijana anayemaliza mafunzo ya jeshi la akiba ni askari kamili,
Amesema mafunzo ya jeshi la akiba yanawajenga vijana katika utimamu wa mwili na kuwakinga na magonjwa yasiyo ya kuambukiza. Amesema mafunzo hayo ya jeshi la akiba yatasaidia Halmashauri ya serikali ya kijiji kupata vijana ambao watakuwa tayari kusaidia katika eneo lao shughuli zote zinazohitaji watu waliopitia mafunzo ya askari wa jeshi la akiba. Amesema hata udahili wa nafasi za kujiunga na jeshi la kujenga taifa ukitokea, lazima vijana hao wa jeshi la akiba wapewe kipao mbele. Vijana hao watasaidia katika shughuli mbalimbali zitakazokuwa zinahitaji usimamizi wa jeshi la akiba kama shughuli za mitihani, na zoezi la sensa ya watu na makazi.
Mh.kayanda amekemea tabia ya watu kuwavunja moyo vijana hao katika ushiriki wa mafunzo ya jeshi la akiba, amesema huo ni upotoshaji na vyema hatua za kisheria zikachukuliwa dhidi ya watu hao ambao hawana nia njema na vijana hao wanaoshiriki mafunzo ya jeshi la akiba. Akizungumzia kuhusu swala la sare kwa vijana hao amesema swala hilo litashughulikiwa mapema ili kuhakikisha vijana wa mafunzo ya jeshi la akiba wanapata sare.
Katika hatua nyingine Mh. Kayanda ametembelea na kutatua mvutano ulikuwepo kati ya serikali ya kijiji na ndg. Patrick vitals ukihusisha makubaliano ya serikali ya Halmashauri ya kijiji wa kuacha umbali wa eneo la mita 10 kila upande ili kuacha nafasi kwenye eneo la korongo la maji katika kitongoji cha upper kitete juu. Mh. Kayanda ameelekeza serikali ya kijiji kusimamia maazimio ya serikali ya kijiji kikamilifu badala na kufanya upendeleo wa utekelezaji wa maazimio hayo ambao upande mmoja wa eneo la shamba la Ndg. Patrick Vitalis ulikuwa umefuata na kusimamia maelekezo ya serikali ya kijiji huku wananchi wengine waliozunguka sehemu ya korongo hilo wakiwa hawajatenga eneo umbali wa mita 10 kila upande.
Mh. Kayanda amekemea tabia ya viongozi wa serikali kuwa na double standard katika usimamiaji na utekelezaji wa maazimio ya serikali ya kijiji. Amesema mambo hayo yanasababisha migogoro, ameelekeza viongozi wa serikali ya kijiji kuweka alama za mipaka katika eneo hilo kuanzia juma lijalo ili kuonesha mipaka wa eneo la hifadhi ya korongo na eneo la shughuli za kibinadamu linapoishia katika kujenga uelewa wa pamoja kwa wananchi.
Naye diwani wa kata ya Mbulumbulu Mh. Eliasi Simpa amempongeza Mh. Kayanda kwa moyo wake wa kupenda kujitoa, amesema wao kama viongozi wa kata ya Mbulumbulu watasimamia na kuhakikisha maelekezo ya serikali yanafanyiwa utekelezaji kikamilifu. Katika hatua nyingine Mh. Simpa ameahidi kusimamia upatikanaji wa sare za vijana wa kike saba wanaoshiriki katika mafunzo ya jeshi la akiba katika kijiji cha Lositete. Amesema mafunzo ya kijeshi ni muhimu na yanasaidia kujenga nidhamu kwa vijana wa kijiji cha Lositete.
Ameongeza kusema mafunzo hayo yanamfanya kijana kuwa muadilifu katika utendaji wa kazi zake binafsi na kazi za umma. Amesema mafunzo ya uaskari yanamfanya kijana kuwa chachu ya maendeleo katika jamii kwa kujihusisha na shughuli za uzalishaji zake binafsi za uzalishaji mali au kufanya shughuli za umma katika Nyanja ya ulinzi.
No comments:
Post a Comment