Kundi la watu wanaotuhumiwa kwa mauaji ya Rais wa Haiti, Jovenel Moise limewaambia wapelelezi kwamba walitaka kumkamata kiongozi huyo na sio kumuua.
Hayo yamebainika katika ripoti iliyotolewa jana na gazeti la Marekani la Miami Herald na mtu wa karibu anayefuatilia mauaji hayo.
Likiwanukuu watu waliozungumza na watuhumiwa 19 wanaoshikiliwa hadi sasa, gazeti hilo limeeleza kuwa lengo lao lilikuwa kumkamata Moise na kumpeleka kwenye Ikulu ya rais.
Duru za karibu na intelijensia zimesema watuhumiwa wawili wenye uraia wa Haiti na Marekani, James Solages na Joseph Vincent wamewaambia wapelelezi kwamba walikuwa wakalimani wa kitengo cha makamandoo wa Colombia ambacho kilikuwa na hati ya kumkamata Moise. Lakini walipofika walimkuta keshakufa.
Wakati huo huo, polisi wa Haiti wamesema wamemkamata raia wa nchi hiyo aliyetumia ndege binafsi kushirikiana na watu wanaotuhumiwa kupanga pamoja na kutekeleza mauaji ya Moise.

No comments:
Post a Comment