Umoja wa Mataifa umeelezea wasiwasi wake kuhusu maelfu ya watu wanaoteseka na njaa katika jimbo la Tigray, kaskazini mwa Ethiopia.
Umoja wa Mataifa umesema licha ya kuwepo hatua ya kusitisha vita, jambo linalofadhaisha zaidi ni ukosefu wa chakula kwa kiwango cha kutisha katika eneo hilo, hali inayotokana na mizozo.
Zaidi ya watu 400,000 wamo katika janga la njaa na wengine wapatao milioni moja na laki nane wanakadiriwa kuingia katika hali hiyo mbaya.
Ramesh Rajasingham, mratibu wa misaada ya dharura katika ofisi ya Umoja wa Mataifa inayoshughulikia masuala ya kibinadamu (OCHA) alikiambia kikao maalum cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwamba idadi ya watu wanaokabiliwa na baa la njaa katika jimbo la Tigray ni kubwa zaidi, kulingana na makadirio mengine.
Amesema maelfu ya watu wamelazimika kuukimbia mzozo huo na watu zaidi ya milioni 5.2 wanahitaji misaada kwa haraka na kwamba idadi kubwa ya watu hao ni wanawake na watoto.

No comments:
Post a Comment