Maambukizi ya Corona nchini Kenya yataongezeka kufikia katikati ya mwezi Julai, 2021, katika wimbi la nne, hii ni kwa mujibu wa Taasisi ya Utafiti wa Kimatibabu nchini humo (KEMRI) ambapo imesema kuwa wimbi hilo la nne ni la Corona ya India tayari limeshaingia nchini Kenya.
Taasisi hiyo ya KEMRI imesema kuwa hatua zilizochukuliwa mwezi Juni huenda zikasaidia kupunguza kusambaa kwa maambukizi hayo na kwamba maeneo yatakayoathirika na wimbi la nne ni Magharibi mwa Kenya, maeneo ya Ziwa Victoria, Nairobi na Mombasa.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu katika Wizara ya Afya nchini Kenya Dkt. Patrick Amoth, amesema kuwa hatua zaidi zinahitajika kuchukuliwa ili kuepusha athari kubwa.
Hadi kufikia sasa jumla ya Kaunti 13 za Magharibi na Bonde la Ufa zimewekewa masharti ya kudhibiti maambukizi ya Corona, ikiwemo kutotoka ndani kuanzia saa 1:00 jioni na kuepusha misongamano kwa namna yoyote ile na hata maeneo ya ibada yamefungwa kwa siku 30.

No comments:
Post a Comment