Search This Blog

Monday, July 26, 2021

Jeshi la Marekani kuondoa Iraq mwisho wa mwaka


Rais wa Marekani Joe Biden anasema vikosi vya Marekani vitamaliza misheni yao ya mapigano nchini Iraq ifikapo mwishoni mwa mwaka huu, lakini wataendelea kutoa mafunzo na kuwashauri wanajeshi wa Iraq.

Tangazo hilo lilikuja baada ya Bwana Biden kufanya mazungumzo na Waziri Mkuu wa Iraq Mustafa al-Kadhimi katika Ikulu ya White House.

Hivi sasa kuna wanajeshi 2,500 wa Marekani nchini Iraq wakisaidia vikosi vya nchi hiyo kukabiliana na wapiganaji waliobaki wa kundi la Islamic State

Idadi ya wanajeshi wa Marekani inaweza kusalia jinsi ilivyo lakini hatua hiyo inaonekana kama jaribio la kumsaidia Waziri Mkuu wa Iraq.

Uwepo wa Marekani nchini Iraq umekuwa swala kubwa tangu jenerali mkuu wa Irani Qasem Soleimani na kiongozi wa wanamgambo wa Kiislamu wa Shia wanaoungwa mkono na Iran kuuawa katika shambulizi la droni ya Marekani mjini Baghdad mwaka jana.

Vyama vya kisiasa vinavyoegemea upande wa Iran vimetaka kuondolewa kwa vikosi vyote kutoka kwa muungano wa kimataifa unaoongozwa na Marekani dhidi ya IS, licha ya tishio linaloendelea kutolewa na kundi hilo la kijihadi la Sunni.

Wapiganaji wa Kishia wakati huo huo wameshtumiwa na Marekani kwa kutekeleza mamia ya mashambulizi ya roketi,na droni dhidi ya vituo vya jeshi la Iraq vinavyotumiwa na wanajeshi wa muungano katika jaribio dhahiri la kuwashinikiza waondoke.

Kwa rais wa Marekani , tangazo hilo linaashiria kumalizika kwa vita vingine vilivyoanza chini ya Rais wa zamani George W Bush. Mwaka huu alisema askari wa Marekani wataondoka Afghanistan na tayari wameondoka nchini humo .

Akiongea katika Ikulu ya White House, Bwana Biden alimwambia mwenzake wa Iraq "ushirikiano wetu wa kupambana na ugaidi utaendelea hata tunapoelekea katika awamu hii mpya."

Bwana Kadhimi alijibu: "Leo uhusiano wetu umekuwa na nguvu zaidi ya hapo awali. Ushirikiano wetu ni kwa uchumi, mazingira, afya, elimu, utamaduni na zaidi." Amesisitiza hakuna vikosi vya kupigana vya kigeni vinahitajika nchini Iraq.

Vikosi vinavyoongozwa na Amerika viliivamia Iraq mnamo 2003 kumpindua Rais Saddam Hussein na kuondoa silaha za maangamizi ambazo hazikuwepo.

Wakati huo Rais George W Bush aliahidi "Iraq huru na yenye amani", lakini iligubikwa na uasi wa kimadhehebu uliosababisha maafa ya watu wengi .

Wanajeshi wa Marekani mwishowe waliondoka mnamo 2011. Walakini, walirudi kwa ombi la serikali ya Iraq miaka mitatu baadaye, wakati wanamgambo wa IS walipovamia sehemu kubwa za nchi.

Kufuatia kushindwa kijeshi kwa IS huko Iraq mwishoni mwa mwaka 2017, vikosi vya Marekani vilibaki kusaidia kuzuia kuzuka tena kwa kundi hilo.

"Jukumu letu nchini Iraq litashughulikia kuendelea kutoa mafunzo, kusaidia, na kushughulikia ISIS," Bwana Biden aliongeza katika mkutano huo.

"Lakini hatutakuwa, mwishoni mwa mwaka, katika opareheni za kivita ."

 



No comments:

Post a Comment

Punguza kilo tano kwa siku saba

  NI watu wachache wanaopenda kunenepa, wengi wanapenda miili ya wastani kwa kuwa  unene si mzuri. Ukiwa mnene si tu kwamba unakaribisha m...