Search This Blog

Thursday, July 29, 2021

DC Babati atangaza Vita kwa wezi wa Miundombinu ya TANESCO.


Na John Walter-Babati

Mkuu wa wilaya ya Babati Lazaro Twange,ametangaza vita dhidi ya waharifu  na watu wanaojihusisha na wizi wa miundombinu ya umeme na miradi ya kimkakati  inayotekelezwa yenye lengo la kuchochea kukua kwa uchumi katika maeneo mbalimbali  wilayani humo.
 
Ametoa kauli hiyo  wakati akiongea na  wakazi wa Mtaa wa  Komoto kata ya Bagara mjini Babati kufuatia watu wasiofahamika kufanya uharibifu  na kuiba chuma katika nguzo kubwa za umeme zinazotoka nchini Tanzania hadi Kenya  na kusababisha  hasara kubwa kwa Tanesco.
 
Twange amesema Serikali haitakuwa na huruma kwa mtu au kikundi cha watu wanaojihusisha na vitendo vya uharifu hasa kwenye miundombinu ambayo inajengwa kwa fedha nyingi za walipa kodi.
Kwa mujibu wa mkuu wa wilaya Lazaro Twange Mradi huo unagharimu zaidi ya shilingi Bilioni 500 za Kitanzania.
 
Amesema, umeme ni nishati muhimu  kwa uchumi wa nchi,kwa hiyo ni wajibu wa kila mmoja kuwa mlinzi na kulinda miundombinu hiyo  inayojengwa kwa lengo la kuchochea na kuharakisha maendeleo.
 
Mkuu wa wilaya, amewataka viongozi na wananchi katika mtaa wa Komoto  na meneo yote ambayo nguzo hizo zimepita kutoa taarifa na kuwafichua watu wanaojihusisha na matukio ya wizi wa miundombinu hiyo ili hatua ziweze kuchukuliwa dhidi yao.
 
Twange ambaye ni mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama,amewaomba watendaji wa wa Serikali ngazi mbalimbali ,wenyeviti wa mitaa na Vijiji kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama ili kukomesha vitendo hivyo vinavyorudisha  nyuma maendeleo.
 
Kwa upande wake afisa Usalama wa  wa shirika la umeme (TANESCO)  mkoa wa Singida Davis Mkwiche  ameeleza kuwa nguzo tisa katika wilaya ya Babati zimeharibiwa na watu wanaodhaniwa kuwa ni wezi ambapo wamekata chuma  ndogo zilizowekwa kuzunguka nguzo hizo.
 
Mradi huo wa kimkakati wa utengezaji wa njia ya  kusafirisha umeme wa Kilovoti 400  unaotekelezwa kutoka Tanzania hadi nchini Kenya upo katika hatua za mwisho za kukamilika kabla ya kukabidhiwa kwa Tanesco
 
Mkwiche amesema uchunguzi wa awali unaonyesha kuwa watu hao baada ya kuiba vyuma huvitumia kutengeneza mikokoteni ambayo inakokotwa na wanyama,mikuki na visu,bangili huku wengine wakiviuza kwa wanaoununua chuma chakavu.
 
Aidha Shirika hilo limeahidi zawadi nono kwa mwananchi atakayetoa taarifa zitakazosaidia kupatikana kwa waharibifu na wezi wa miundombinu hiyo na kuwafichia siri watoa taarifa.
 
Amesema,serikali imekuwa ikijitihadi sana kuboresha miundombinu yake,hata hivyo baadhi ya watu wachache wanarudisha nyuma juhudi  hizo  kwa kuharibu kwa makusudi miundombinu ya umeme na kuisababishia Serikali hasara kubwa.
 
Ameiomba jamii kushirikiana na Tanesco kulinda na kuwa walinzi wa  miundombinu ya umeme kwani nishati hiyo ina umuhimu mkubwa kwa maendeleo ya mtu mmoja mmoja na taifa.
 
Afisa Upelelezi kutoka jeshi la Polisi wilaya ya Babati Said Ramadhani amesema kosa la kuharibu au kuiba miundombinu ya Tanesco ni Uhujumu Uchumi ambapo adhabu yake ni kifungo na usafiri uliotumika katika uhalifu huo hutaifishwa kwa mujibu wa sheria ya mwaka 1984 iliyofanyiwa marejeo mwaka 2002 na 2019.

 



No comments:

Post a Comment

Punguza kilo tano kwa siku saba

  NI watu wachache wanaopenda kunenepa, wengi wanapenda miili ya wastani kwa kuwa  unene si mzuri. Ukiwa mnene si tu kwamba unakaribisha m...