Mchekeshaji wa Marekani Bill Cosby ameondoka gerezani saa chache baada ya hukumu yake ya unyanyasaji wa kingono kutenguliwa na Mahakama ya juu zaidi ya Pennsylvania.
Majaji walisema kulikuwa na "ukiukaji wa utaratibu" na upande wa mashtaka, lakini walikiri uamuzi wao ulikuwa sio wa kawaida.
Bwana Cosby, 83, alitumikia zaidi ya miaka miwili ya kifungo cha miaka mitatu hadi 10 katika gereza la serikali karibu na Philadelphia.
Mnamo 2018 alipatikana na hatia kumpa dawa za kulevya na kisha kumdhulumu kingono mchezaji wa zamani wa mpira wa kikapu Andrea Constand.
Bwana Cosby ni maarufu sana kwa maigizo ya vipindi vya runinga hasa kwenye kipindi chake cha mwaka wa 1980 The Cosby Show na alijulikana kama "Baba wa Marekani".
Makumi ya wanawake wamemshtaki Bw Cosby kwa dhuluma za kingono, lakini alishtakiwa tu kwa jinai kwa tukio dhidi ya Bi Constand.
Kuhukumiwa kwake mnamo 2018 kulionekana sana kama wakati muhimu kwa harakati ya #MeToo.
Katika uamuzi uliotolewa Jumatano, mahakama ya juu kabisa ya Pennsylvania iligundua kulikuwa na "ukiukaji wa utaratibu" kwa sababu mawakili wa Bw Cosby walikuwa wamefanya makubaliano na mwendesha mashtaka wa zamani wa serikali kwamba hatashtakiwa katika kesi hiyo.
Muigizaji huyo wa zamani alionekana dhaifu wakati akitembea polepole kwenda kwa waandishi wa habari waliokuwa wakimsubiri nje ya nyumba yake muda mfupi baada ya kutolewa gerezani.

No comments:
Post a Comment