Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Tamisemi Ummy Mwalimu ameitaka jamii ya Watanzania kuendelea kutunza mazingira yanayowazunguka ili kusaidia udhibiti wa mabadiliko ya tabia nchi.
Akizungumza wakati wa hafla ya utoaji tuzo kwa washindi kumi wa shindano la Mazingira yangu ni Wajibu lililoandaliwa na Taasisi ya Feet Waziri Ummy amesema mazingira ni kila kitu, hivyo yakilindwa yatasaidia kuimarisha uchumi.
Hafla hiyo pia imehudhuriwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Balozi Liberata Mulamula ambaye ameikumbusha jamii umuhimu wa kutunza mazingira huku Balozi wa Ufaransa nchini Tanzania Frederick Claiver akibainisha namna nchi yao inavyounga mkono juhudi za kupinga mabadiliko ya tabia nchi.
Katika kuionesha jamii ukubwa wa tatizo hilo na hatimaye kuweza kuchukua hatua, Taasisi ya FEET iliandaa shindano la Mazingira yangu ni Wajibu kuhamasisha vijana kutunza mazingira kupitia mitandao ya kijamii ili kila mmoja aone ana wajibu huo.
Rebeca Muna na Godfrey Haule ni baadhi ya washindi wa shindano hilo la Mazingira yangu ni Wajibu wangu ambao wanaeleza namna shindano hilo lilivyobadilisha mitazamo yangu.
Mabadiliko chanya ya kuhifadhi mazingira na kudhibiti mabadiliko ya tabia nchi ni jukumu la kila mtu.

No comments:
Post a Comment