Nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, maafisa watatu wa jeshi wamekamatwa kuwekwa chini ya ulinzi kwenye ofisi ya mwendesha mashtaka mkuu wa korti ya kijeshi huko Ituri, mashariki mwa nchi hiyo.
Maafisa hao wanashtakiwa kuongeza idadi ya wanajeshi wa vikosi vilivyo kwenye mapambano wakati huu ambapo kumetangazwa utawala wa kijeshi wa muda kwenye mkoa huo wa kaskazini mashariki mwa Kongo.
Miongoni mwa maafisa waliokamatwa ni mmoja mwenye cheo cha luteni kanali, ambaye ni naibu mkurugenzi anayesimamia utawala wa mkoa wa kijeshi wa 32 huko Bunia.
Waliongeza idadi ya uongo ya wanajeshi ili kuchukua mishahara yao
Pia wamo mameja wawili, mmoja akiwa kiongozi wa ofisi ya malipo ya mkoa na mwenzake akiwa mkuu wa kikosi kilicho katika uwanja wa mapambano huko Boga katika eneo la Irumu.
Maafisa hao wanashukiwa kuongeza idadi ya wanajeshi ili kujichukulia ongezeko la mishahara kwa kughushi. Kwa sasa, uchunguzi unaendelea ili kujuwa undani wa kadhia hiyo, kama alivyoeleza Luteni Jules Ngongo, msemaji wa jeshi katika eneo la Ituri:
"Sheria ya kijeshi inayoiunga mkono amri katika wakati huu wa muzingiro imewashikilia maafisa watatu wanaofanya kazi katika utawala. Kwa sasa uchunguzi unaendelea na ikiwa wengine hawataki kubadilika, watabadilishwa na mabadiliko yanayotetewa na Kamanda Mkuu wa Jeshi, mkuu wa Nchi," alisema Luteni Jules Ngongo.
Hayo yamejitokeza wakati Rais Félix Tshisekedi bado yupo ziarani upande huo wa mashariki, ambapo alibaini siku chache zilizopita, kuwepo na hali ya udanganyifu ndani ya jeshi la kitaifa.
Serikali iendelee kufanya uchunguzi ili kuchukua hatua zaidi
Shirika la kiraia la Ituri limeridhishwa na hatua hii ya kuwashikilia maafisa wa kijeshi kwa tuhuma za ufisadi, ila limeomba kuwe na uchunguzi zaidi ili kuwafikisha wahusika mbele ya mahakama.
"Tunaomba serikali iendelee kutafuta wengine wanaoshiriki na hao viongozi wanaoleta sura mbaya kwa Kongo. Kama leo mauaji yanazidi ni kwa sababu kuna watu katika jeshi wanaowasaidia. Sisi tunaomba wahukumiwe. Inabidi baba wa taifa aongeze jeshi na vifaa vinavyoweza kusaidia kufukuza wale wanamgambo," alisema Lossa Dekhana.
Mikoa ya Ituri na Kivu ya Kaskazini imekuwa chini ya utawala wa muda wa kijeshi tangu Mei 6, ili kujaribu kumaliza ghasia na ukosefu wa usalama katika mikoa hiyo ya mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

No comments:
Post a Comment