Rais wa Marekani Joe Biden amewaahidi viongozi wa juu wa Afghanistan ushirikiano endelevu hata wakati ambapo anaelekea kukamilisha mchakato wa kumaliza vita vya muda mrefu vya Marekani nchini Afghanistan chini ya kiwingu cha kuongezeka machafuko nchini humo.
Rais Biden ambaye aliwakaribisha Ikulu mjini Washington Rais Ashraf Ghani na mwenyekiti wa baraza kuu la maridhiano ya kitaifa nchini Afganistan Abdalla Abdalla, ameahidi kwamba Marekani itaisadia Afghanistan lakini pia akasisitiza kwamba ni wakati wa jeshi la nchi yake kukaa kando.
Rais Biden amewatanabaisha viongozi hao kwamba Waafghanistan watapaswa kuamua mustakabali wao. Kabla ya mkutano na rais Biden, Rais Ghani na Abdalla Abdalla walikutana kwanza na waziri wa ulinzi Lloyd Austin katika ofisi za wizara ya hiyo, Pentagon.
Ziara ya viongozi hao wa Afghanistan nchini Marekani imekuja wakati serikali ya rais Joe Biden ikiwa imeimarisha mipango ya kuondowa kikosi chake kabla ya tarehe ya mwisho iliyowekwa ya Septemba 11.

No comments:
Post a Comment