Search This Blog

Monday, May 24, 2021

Watu 15 wafariki dunia baada ya mlipuko wa Volkano DRC

 


Takriban watu 15 wamethibitishwa kufariki kutokana mlipuko wa volkano uliotokea katika Mlima wa Nyiragongo, mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC) lakini huenda idadi ya vifo ikaongezeka wakati maafisa wakiyafikia maeneo yaliyoathirika zaidi.

Volkano ililipuka katika mlima Nyiragongo una kumwaga ujiuji wa moto ama lava uliolifanya anga kuwa jekundu Jumamosi, lakini lava hiyo haikuhfika katika mji wa Goma unaokaliwa na watu milioni mbili kusini mwa mlima huo.

Wakazi wa vijiji vya karibu na mlima huo pamoja na mji Goma ambao waliyakimbia makaazi yao kwa hofu ya mlipuko huo wameanza kurejea huku wengi wao wakiwasaka jamaa zao waliopotea.

Watu tisa miongoni mwa waliothibitishwa kufa, walipoteza maisha katika ajali za barabarani wakati watu walipokuwa wakihaha kukimbia ili kuokoa maisha yao.

Wanne walikufa walipokuwa wakijaribu kutoroka gerezani huku wawili wakiungua hadi kufa, alisema msemaji wa serikali Patrick Muyaya Jumapili.

Zaidi ya watoto 170 wanahofiwa kupotea na wengine 150 wametengana na familia zao, kulinga na Shirika la Watoto la Umoja wa Mataifa (Unicef) ambalo linasema litaweka vituo vya kuwapokea watoto watakaopatikana wakiwa peke yao.

Lava iliishia karibu na wilaya ya Buhene, viungani mwa mji wa Goma na kuangamiza mamia ya nyumba na hata majengo makubwa. Ukarabati unatarajiwa kuchukua miezi kadhaa.

"Nyumba zote zilizopo katika wilaya ya Buhene zimeungua," Innocent Bahala Shamavu aliliambia shirika la habari la kimataifa la Associated Press.

Kwengineko, lava ilikatiza katika moja ya barabara kuu inayounganisha Goma na mji wa Beni, ambayo ni njia muhimu ya usambazaji wa misaada.

Hata hivyo, uwanja wa ndege wa wa mji wa Goma haukuguswa na lava, kinyume na ripoti za awali kwamba uliathiriwa.

Mitikisiko ilisikika baada ya kulipuka kwa volkano hiyo, alisema Bw Muyaya. "Watu wanashauriwa kuendelea kuwa macho, kuepuka safari zisizo za lazima, na kufuata maelekezo," ulisema ujumbe wake wa Twitter.

Mlima huo wa volkano hiyo uliopo kilomita 10 (maili sita) kutoka Goma, ulilipuka mara ya mwisho mwaka 2002 na kusababisha vifo vya watu250 huku watu wengine 120,000 wakiachwa bila makazi.

Wakazi wa Goma walianza kuzikimbia nyumba zao kabla serikali kutangaza mpango wa namna ya kuondoka katika mji huo.

Umati wa watu ulionekana usiku ukiondoka kwa miguu huku baadhi yao wakiwa wamebeba magodoro na mali zao nyingine.



No comments:

Post a Comment

Punguza kilo tano kwa siku saba

  NI watu wachache wanaopenda kunenepa, wengi wanapenda miili ya wastani kwa kuwa  unene si mzuri. Ukiwa mnene si tu kwamba unakaribisha m...