Serikali ya Tanzania itajenga chuo cha ufundi Mkoa wa Dodoma chenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 5000 ili kuongeza wigo na fursa za upatikanaji wa ujuzi na maarifa.
Akizungumza leo Jumamosi Mei 29, 2021 katika hafla ya utiaji saini mkataba wa ujenzi wa chuo hicho uliofanyika jijini Dodoma, katibu mkuu wa Wizara wa Elimu, Dk Leonard Akwilapo amesema ujenzi wa chuo hicho utagharimu zaidi ya Sh17 bilioni kupitia mradi wa Kukuza Ujuzi na Stadi za Kazi (ESPJ) unaosimamiwa na wizara hiyo.
Katibu Mkuu huyo ameitaka kampuni iliyoshinda zabuni ya ujenzi wa chuo hicho ya CRJE East Africa Ltd kuhakikisha inakamilisha ujenzi huo ndani ya miezi 18 kama mkataba unavyoonyesha.
“Leo tumesaini mkataba wa ujenzi wa chuo cha ufundi Dodoma, ni matarajio yangu kitakamilika kwa wakati naubora unaotakiwa ili malengo ya kuanzishwa kwa chuo hiki yaweze kutimia,” amesema Dk Akwilapo.
Meneja wa kampuni ya CRJE East Africa Ltd tawi la Tanzania, Xu Cheng ameahidi kutekeleza mradi huo kwa ubora unaokubalika na kuhakikisha unakamilika kwa wakati uliopangwa.
Mradi huo utahusisha ujenzi wa miundombinu ya jengo la utawala, ofisi za idara, nyumba za watumishi, mabweni, zahanati, vyoo vya wanafunzi na watumishi, karakana tatu na kituo cha kupoza umeme.

No comments:
Post a Comment