Viongozi kadhaa ulimwenguni, wameelezea kushitushwa na kifo cha aliyekuwa rais wa Chad, Idriss Deby Itno, kilichotangazwa jana, muda mfupi baada ya kutangazwa mshindi wa uchaguzi, kwa muhula wa sita madarakani.
Ofisi ya Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa, mkoloni wa zamani wa Chad, imekielezea kifo cha Deby, kama pigo kwa juhudi za amani, katika ukanda wa Sahel.
Wizara ya Mambo ya Kigeni ya Marekani, imesema nchi hiyo inaungana na watu wa Chad, kwenye wakati huu wa huzuni, huku ikiunga mkono kipindi cha mpito, kwa mujibu wa katiba ya Chad.
Hata hivyo, tayari jeshi limevunja serikali na bunge, na kumtangaza mtoto wa kiume wa Deby, Jenerali Mahamat Deby, kuchukuwa madaraka, kwa kipindi cha miezi 18 ya utawala wa mpito.
Mkuu wa Muungano wa Afrika, Moussa Fakki Mahamat, mwenyewe akiwa waziri mkuu wa zamani wa Chad, amesema kifo cha Deby, kimemchukuwa mwanajeshi shupavu wa nchi yake.
Jeshi linasema Deby, aliyeingia madarakani miongo mitatu iliyopita kwa mapinduzi, alikufa kutokana na majeraha aliyopata, akiwa uwanja wa mapambano na waasi, mpakani mwa nchi hiyo na Libya, wiki iliyopita.

No comments:
Post a Comment