Baada ya wabunge kadhaa kulia kuhusu mikopo ya elimu ya juu na uhaba wa vyumba vya madarasa kwa shule za sekondari, Serikali imeahidi kuzishughulikia changamoto hizo.
Kwenye mkutano wa Bunge unaoendelea jijini hapa, wabunge wamelalamika kuhusu ulipaji wa deni la elimu ya juu, hasa kwa wanufaika ambao hawajapata ajira kuitaka Serikali kuangalia upya utaratibu uliopo.
Wabunge hao pia walizungumzia changamoto ya wanafunzi wengi wa kidato cha kwanza kuchelewa kujiunga shule kutokana na uhaba wa madarasa.
Akijibu hoja hizo, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa jana wakati anaahirisha mkutano huo wa Bunge la 12, alisema Serikali inafarijika na inapokea kwa mikono miwili michango yenye afya na tija kuhusu hatma ya mikopo inayotolewa kwa miaka 15 ya uwapo wa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB).
“Nilihakikishie Bunge lako tukufu kwamba Serikali ipo tayari kuendelea kujifunza kutoka kwa wabunge na wananchi wote kuhusu namna bora zaidi ya kuufanya mfuko huu uwe endelevu na wenye manufaa katika ujenzi wa uchumi wa nchi yetu,” alisema Waziri Mkuu.
Vilevile, aliiagiza Wizara ya Elimu, kushirikiana na HESLB kurahisisha urejeshaji wa mikopo kwa wanufaika waliojiajiri na waliopo sekta binafsi kwa kutoa elimu kwa umma kuhusu haki na wajibu wa mnufaika na mwajiri.
ADVERTISEMENT
Majaliwa aliwasihi wanufaika wote, hasa ambao hawajajitokeza kuanza kurejesha, wafanye hivyo mara moja na kuwaomba waajiri kutoa kipaumbele kwenye makato ya mikopo hiyo.
Waziri Mkuu pia alizungumzia mpango wa kumaliza uhaba wa vyumba vya madarasa kwa shule za sekondari.
Alisema mwaka jana Benki ya Dunia iliidhinisha mkopo wa dola 500 milioni za Marekani, sawa na Sh1.2 trilioni kwa ajili ya kuboresha elimu ya sekondari.
Alisema mradi huo wa miaka mitano (2020/21 hadi 2025/26) utakuwa mwarobaini wa uhaba wa miundombinu ya sekondari, kwani shule mpya 1,026 zitajengwa nchini.
Alisema shule mpya 26 zitakuwa za bweni zenye uwezo wa kupokea kati ya wanafunzi 1,000 hadi 1,500 kila mkoa na zitajengwa kwa awamu tatu.
Majaliwa alisema shule mpya 1,000 za kutwa zenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 400 kila moja zitajengw a maeneo tofauti.
“Shule hizo zitajengwa kwenye kata 718 zisizo na sekondari na maeneo yaliyoelemewa na idadi kubwa ya wanafunzi. Hivyo, nitumie nafasi hii kuwaelekeza viongozi na watendaji wa Serikali za Mitaa wasimamie kikamilifu utekelezaji wa mradi huu ili kufikia malengo yaliyokusudiwa,” alisema.
Spika Job Ndugai alikuwa miongoni mwa wabunge waliolia na mikopo hiyo, akisema imekuwa biashara. Alikuwa akiunga mkono hoja iliyotolewa na Mbunge wa Singida Kaskazini, Ramadhan Ihondo, aliyependekeza isiwe na riba na muda wa kurejesha uongezwe.

No comments:
Post a Comment