Waziri Mkuu wa Italia Giuseppe Conte ameponea chupuchupu kura muhimu ya kuwa na imani naye katika Baraza la Seneti usiku wa kuamkia leo, inayomruhusu kuendelea kuiongoza serikali yake tete ya muungano.
Lakini ameshindwa kupata uungwaji mkono wa kuaminika anaohutaji kutoka kwa wabunge ili kumsaidia kuiongoza nchi ambayo uchumi wake umeporomoka kutokana na janga la corona. Alipigiwa kura 156 dhidi ya 140.
Wajumbe 16 hawakupiga kura. Wingi wa kura zinazohitajika katika Seneti ni 161, kwa hiyo ili kupitisha sheria muhimu, ikiwemo msaada wa kuufufua uchumi wa Italia ulioathirika pakubwa, Conte atakabiliwa na uwezekano wa kuwategemea wabunge walioko nje ya serikali yake ya muungano.
Waziri Mkuu huyo amesema sasa lengo lake sasa ni kuikabili hali ya dharura ya kiafya na mgogoro wa kiuchumi. Kama angepoteza kura hiyo, Conte angehitajika kujiuzulu.

No comments:
Post a Comment