Na Hamisi Nasri, Masasi
HALMASHAURI ya wilaya ya Masasi mkoani Mtwara imetoa mikopo ya yenye jumla ya Sh.191.2 milioni kwa vikundi 52 vya ujasiliamali vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu wilayani humo fedha hizo ni zamapato ya ndani
Aidha,vikundi hivyo vimepewa angalizo kuhusu kufanya marejesho kwa wakati ili kutoa wigo kwa wengine kuweza kupata fedha hizo.
Mkopo huo ulitolewa jana mjini Masasi katika ukumbi wa zamani wa halmashauri hiyo na kwamba utekelezaji huo ni agizo la Serikali la kutenga asilimia 10 ya mapato ya ndani ya kila halmashauri kwa ajili ya kuvipa vikudni.
Akizungumza katika hafla ya utoaji wa mkopo huo, mkuu wa wilaya ya Masasi, ambaye ndiye aliyekuwa mgeni rasmi , Selemani Mzee kwa niaba ya mkuu wa mkoa wa Mtwara, Gelasius Byakanwa alivipongeza vikundi hivyo kwa kupata mkopo huo na kuvikumbusha umuhimu wa kufanya marejesho kwa wakati.
Alisema kuwa wanachama wa vikundi hivyo wanapaswa kwenda kutumia mkopo huo kwa malengo yaliyokusudiwa jambo ambalo litaweza kuleta tija kwa uhai wa vikundi vyao na kujiongezea kipato ndni ya familia zao.
“Mikopo hii msidhani kama ndio nafasi kwenu ya kufanya mambo yenu binafsi bali mmepewa kwa lengo la kuinua mitaji ya biashara zenu hivyo mkaitumie kwa malengo yaliyokusudiwa ili iweze kuwainua kiuchumi,”alisema Mzee
Kwa upande wake, kaimu mkurugenzi mtendaji wa halmashauri hiyo ya wilaya ya Masasi,Ryoba Magabe alisema halmashauri ya wilaya ya Masasi ina ujumla ya vikundi hai vya kiuchumi 1,009 vilivyoandikisha katika daftari la halmashauri.
Alieleza kwamba vikundi hivyi vinaendelea kupatiwa usaidizi wa mitaji kupitia mikopo yenye masharti nafuu
“Kuanzia mwaka 2015/2016 hadi Januari 2020/ 2021 jumla ya vikundi 497 vya wanawake,vijana na watu wenye ulemavu tayari vimeshapatiwa mikopo yenye jumla ya thamani ya zaidi ya sh.1.1 bilioni na fedha kwamba hizo zote ni kutoka kwenye mapato ya ndani,”alisema Magabe
Naye afisa maendeleo ya jamii wa halmashauri hiyo, Neema Joseph alisema licha ya halmashauri kutoa kiasi hicho cha mkopo bado inadai jumla ya sh. 200 milioni kwa baadhi ya vikundi kwa kipindi kilichopita.
Alisema mwezi Julai Disemba 2020 halmashauri ilipokea maombi ya mikopo kutoka katika vikundi 83 vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu mikopo hiyo ilikuwa na thamani ya sh. 637,537,720 baada ya kamati ya huduma za mikopo vikundi 52 ndio vilikidhi vigezo ya kupata fedha hizo.
Akizungumza kwa niaba ya wanachama wa vikundi hivyo Satma bakiri kutoka kikundi cha Maendeleo kilichopo katika kijiji cha Mikangaula alisema kuwa wanaipongeza halmashauri hiyo kwa kuwapatia mkopo huo na kwamba wanauhakika wa kufanya marejesho kwa wakati kwani kupitia mmkopo wataweza kuinua uchumi katika familia zao.

No comments:
Post a Comment