Na John Walter-Manyara
Wakazi wa mkoa wa Manyara na watanzania kwa ujumla wamekumbushwa kwamba sheria ya ardhi Cap 113 na sheria ya ardhi ya vijiji Cap 114 haziwapi mamlaka wenyeviti wa mitaa, vitongoji na vijiji kuuza ardhi.
Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa Takukuru mkoa wa Manyara Holle Makungu baada ya baadhi ya wenyeviti mkoani humo kuuza ardhi kinyume na taratibu na kusababisha migogoro katika maeneo hayo.
Makungu amewaambia wananchi kuwa mamlaka ya kuuza ardhi kwa maana ya ardhi ya kijiji yapo mikononi mwa mkutano mkuu wa kijiji kwa ekari zisizozidi hamsini (50) na kushuhudia mauziano kwa mujibu wa sheria hizo yapo kwa ofisi ya watendaji na sio wenyeviti.
Amesema kwa msingi huo mauziano yanayofanywa kupitia wenyeviti ni batili na hayana nguvu ya kisheria, hivyo wananchi wawe waangalifu na vitendo vya baadhi ya wenyeviti wachache wasio waadilifu wanaojihusisha na uuzaji wa ardhi.
Makungu amewaambia waandishi wa habari kuwa Katika kipindi cha Mwezi Oktoba hadi Desemba 2020 Takukuru mkoa wa Manyara ilipokea Malalamiko 208 ambapo kati ya hayo 127 yalihusiana na makosa ya rushwa na malalamiko 81 yalihusu makosa mengine ambapo walalamikaji walishauriwa na kuelekezwa katika ofisi husika kwa ajili ya utatuzi wa malalamiko yao.
Makungu amesema kesi mbili zilizokamilika watuhumiwa wote walikutwa na hatia huku kesi mbili mpya zikiendelea mahakamani.

No comments:
Post a Comment