Na Ahmad Mmow, Lindi.
Waandishi wa habari mkoani Lindi wameshauriwa kufanya kazi nyingine za uzalishaji mali badala ya kutegemea kazi moja ya uandishi ili waweze kujinasua katika hali ngumu ya maisha.
Ushauri huo ulitolewa jana, na mbunge wa Lindi mjini, Hamida Abdallah alipozungumza na baadhi ya waandishi wa habari waliopo katika manispaa ya Lindi. Kikao baina ya mbunge huyo na waandishi hao kilifanyika mjini Lindi.
Mbunge Hamida alisema waandishi wa habari, hasa wa Lindi hawana sababu ya kuendelea kulalamika ugumu wa maisha na kuwa wanyonge kutokana kutokuwa na mikataba na vyombo wanavyofanyia kazi na kulipwa ujira mdogo usio kidhi gharama za maisha yao ya kila siku. Badala yake watumie fursa zinazo wazunguka ili kujiongezea vipato.
Alisema itakuwa vigumu kwao kujikwamua kutoka kwenye ugumu wa maisha iwapo wataendelea kutegemea kazi moja ya uandishi. Bali wafanya kazi mbadala kupitia fursa zilizopo katika manispaa ya Lindi na mkoa wa Lindi kwa jumla.
Alisema sekta ya kilimo ni miongoni mwa maeneo ambayo yanayo weza kutumiwa na waandishi hao kufanya kazi mbadala inayoweza kuwaingizia kipato. Kwahiyo wasisite kuwekeza kwenye kilimo. Hasa ikizingatiwa kwamba halmashauri ya manispaa ya Lindi na mkoa wa Lindi ina ardhi nzuri inayofaa kwa kilimo.
" Lakini pia mkoa wa Lindi unazalisha mazao mengi ya kilimo ambayo mnaweza kuyapandisha thamani mkiamua kuwekeza kwenye viwanda vidogo. Shughuli za kufanya ni nyingi usitegemee mpaka upate habari fulani ukirusha ndipo upate fedha, hauwezi kutoka," Hamida alisisitiza na kuonya.
Alisema kwa sasa miundo mbinu ya barabara imeboreshwa na kurahisisha usafiri wa kutoka eneo moja kwenda eneo jingine. Kwahiyo hawana budi kutumia fursa hiyo kwa kuwekeza katika sekta za kilimo na biashara. Kwani kwa kufanya hivyo watatengeneza ajira hata kwa watu wengine. Kwakuwa itakuwa rahisi kusafirisha mazao na bidhaa watakazo tengeneza.
Alionya kuwa kutokana na hali ya maisha kubadilika siku hadi siku wana kila sababu ya kubadilika ili kuendena na hali ya wakati husika. Badala ya kuishi kwa mazoea na kuendelea kulalamika.
Aidha mbunge huyo wa jimbo la Lindi mjini aliwaasa wajiandae kutumia vema fursa zitakazo tokanana uwepo wa mtambo wa kuchakata gesi asili ambao unatarajiwa kujengwa katika manispaa ya Lindi mitaa ya Likong'o na Mto mkavu. Akibanisha kwamba serikali imedhamiria kutekeleza mradi huo.
Awali waandishi hao walimueleza mbunge huyo kwamba miongoni mwa changamoto wanazo kutananazo ni waandishi wengi kutokuwa na mikataba na vyombo wanavyofanyia kazi. Lakini pia wanalipwa ujira mdogo usio lingana na gharama za uendeshaji maisha ya kila siku. Hali ambayo inasababisha wawe na maisha magumu.

No comments:
Post a Comment