Na Ahmad Mmow, Lindi.
Katika kutekeleza agizo la waziri Mkuu wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, mheshimiwa Kassim Majaliwa na kuunga mkono juhudi za serikali na wananchi. Mbunge wa jimbo la Lindi, Mheshimiwa Hamida Mohammed Abdallah amemabidhi saruji na matofali kwa shule za sekondari Ngongo, Mitwelo na shule ya msingi Mtanda.
Jana akizungumza kwa nyakati na maeneo tofauti katika shule hizo baada ya kukabidhi mifuko 70 ya saruji na tofali 400 kwa shule ya sekondari ya Ngongo, mifuko 30 ya saruji kwa shule ya msingi Mtanda na mifuko 50 ya saruji na matofali 300 kwa shule ya sekondari ya Mitwelo, mheshimiwa Hamida alisema huo ni utekelezaji wa agizo la waziri mkuu na kuunga mkono nguvu za wananchi kutatua changamoto ya upungufu wa vyumba vya madarasa.
Alisema yeye kama Mbunge wa jimbo la Lindi licha ya kutekeleza agizo la waziri mkuu kwamba muhula wa masomo utakaoanza mwezi Januari 2021 kusiwe na mwanafunzi atakaye shindwa kuanza masomo kwa sababu ya kukosa vyumba vya madarasa, lakini pia yeye hapendi kwenye jimbo hilo wanafunzi washindwe kuanza masomo kutokana na changamoto hiyo.
Alisema ataendelea kutekeleza ilani ya uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi( CCM) na ahadi zake binafsi alizoahidi wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu wa mwaka 2020 kwa wananchi na ataendelea kusimamia kuhakikisha yote aliyoahidi anatekeleza ndani ya kipindi chake cha ubunge( miaka mitano).
Alibanisha kwamba atafuatilia na kutembelea taasisi za umma zinazotoa huduma mbalimbali kwa wananchi ili kila taasisi iweze kutatua changamoto za wananchi kupitia huduma inazotoa. Kwani huo ni miongoni mwa wajibu wake wa msingi kwa wananchi anao wawakilisha.
Mbunge Hamida katika maelezo yake aligusia watoto wenye mtindio wa ubongo na walemavu. Alisema kuna haja ya kuyatupia macho makundi hayo ili yapate elimu. Kwani walemavu wakipata elimu wataweza kujisaidia na kuepuka utegemezi uliopitiliza. Huku akiutaja mtaa wa Ng'apa, manispaa ya Lindi kuwa ni miongoni mwa maeneo yenye watoto wengi wenye tatizo la Mtindio wa ubongo.
Mbali na hayo Mbunge huyo, alisema kasi aliyoanza nayo haitakoma hadi ahadi zake zitekelezwe. Na kwamba hapendi kupelekewa wala kusikiliza majungu. Kwahiyo wenye fikra za kumpelekea majungu na fitna hawana nafasi katika uongozi wake.
" Muda huu sio wakupeana mipasho na kutupiana vijembe, ni muda wa kuwatumikia wananchi wa Lindi. Mipasho, vijembe na majungu sio mahitaji ya wananchi wa jimbo la Lindi. Wanataka kutatuliwa kero na changamoto zinazo wakabili. Kwahiyo mambo hayo hayana nafasi kwangu," alisema Mbunge Hamida.
Mbunge huyo katika kile kinachoonekana kwamba anadhamira ya dhati yakushughulikia kero na changamoto alisema hatakuwa na amani na furaha iwapo katika kipindi chake cha uongozi atashindwa kutekeleza ahadi zake zote.
Kwa upande wake kaimu ofisa elimu sekondari wa halmashauri ya manispaa ya Lindi ambaye ni ofisa utamaduni na michezo wa halmashauri hiyo, mwalimu Maneno Juma alisema katika ukaguzi waliofanya wamebaini kwamba vinahitajika vyumba nane vya madarasa ili kuwezesha wanafunzi wote kusoma ndani ya vyumba vya madarasa.
Mwalimu Juma alisema miongoni mwa vyumba hibyo ni kwamba vipo vyumba vinavyohitaji kukarabatiwa na vingine kujengwa. Huku akiweka wazi kwamba ifikapo Januari 2021 vyumba vyote vitakuwa vimekamilika.

No comments:
Post a Comment