Search This Blog

Sunday, December 6, 2020

Serikali Lindi yawashukuru viongozi wa dini, manispaa yafanikiwa kupima VVU watu 16,058


Na Ahmad  Mmow, Lindi.

Serikali Lindi wilayani Lindi imewashukuru viongozi wa dini wilayani humo kwa kushiriki kikamilifu mapambano dhidi ya UKIMWI na ukatili wa kijinsia.

Shukrani na pongezi hizo zilitolewa jana na mkuu wa wilaya ya Lindi, Shaibu  Ndemanga wakati wa maadhimisho ya siku ya UKIMWI duniani nna uzinduzi wa maadhimisho ya siku kumi na sita za kupambana na ukatili wa kijinsia. Uzinduzi ambao umefanyika katika uwanja wa mpira wa miguu wa Ilulu uliopo katika manispaa ya Lindi.

Ndemanga alisema ushiriki wa viongozi wa dini katika mapambano hayo umechangia kupunguza kiwango cha maambukizi ya Virusi Vya UKIMWI( VVU) na vitendo vya ukatili wa kijinsia katika wilaya hiyo iliyopo katika mkoa wa Lindi.

Alisema hali ya awali kabla ya viongozi wa dini kushiriki mapambano kama ilivyo sasa, kasi ya maambukizi ya VVU  na ukatili wa kinjisia ilikuwa kubwa. Hata hivyo kuingia kwa viongozi hao kwenye mapambano kumechangia kwakiasi kikubwa kupunguza kasi hiyo.

Alitoa wito kwa viongozi hao waendelee kushiriki kikamilifu mapambano hayo ili jamii iweze kunusurika na madhara ya maambukizi ya VVU na ukatili wa kijinsia. Kwani kwa ushirikiano na nguvu za pamoja kuna uwezekano wa kushinda vita hiyo.

Aidha Ndemanga alitoa wito wakuwepo vituo maalumu ambavyo vitakuwa na wataalamu au maofisa wa idara zinazohusika kuwasaidia waathirika na wanatendewa vitendo vya ukatili wa kijinsia na unyanyasaji ili kuwarahisishia upataji huduma.

" Nashauri utafutwe uwezekano wa kuwa na senta ( kituo ) maalumu zitakazo jumuisba wataalamu na maofisa wa idara hizo. Kwasasa nikama wanaohitaji huduma wanachoshwa, dawati la jinsia wapo eneo jingine, ustawi wa jamii eneo jingine," Ndemanga alisisitiza.

Kwaupande wake mratibu wa UKIMWI wa halmashauri ya manispaa ya Lindi, Dkt Zulfa Msami alisema mkoa wa Lindi ni miongoni mwa mikoa inayoonesha mafanikio katika kupambana na UKIMWI kwa kiwango kikubwa. Kwani ina kiwango kidogo cha maambukizi.

Kuhusu wilaya ya Lindi, Dkt Msami alisema halmashauri ya manispaa ya Lindi kwa kipindi cha kuanzia Januari hadi Oktoba 2020 imefanikiwa kupima VVU kwa watu 16,058. Kati ya hao wanaume ni  6,905 sawa na asilimia 43 na wanawake ni 9,153 ambao nisawa na asilimia 47.

Alisema katika upimaji huo waliokutwa ya VVU ni  wanume 262 na wanawake 360 ambao jumla yao ni 622. Akibainisha kwamba upimaji umelenga makundi yenye uwezekano wakuwa na maambukizi(Index testing).

Dkt Msami pia litoa wito kwa watu wanaoishi na VVU nakutumia dawa za kufubaza VVU( ARVs ) na wananchi wote kwamba zimeanza kutolewa ARV kwa wateja wao kwa miezi mitatu. Utaratibu ambao hautawahusu wajawazito, watoto wa chini ya miaka mitano, walio kwenye dawa za mstari wa pili na ambao hawatakidhi vigezo vya kitaalamu.

Mtatibu huyo wa UKIMWI aliwakumbusha wataalamu kufuatilia kwa karibu  mwenendo wa huduma za tiba kwa wagonjwa ili waweze kuchukua hatua pale yanapojitokeza matatizo ya kitaalamu na kiafya.



No comments:

Post a Comment

Punguza kilo tano kwa siku saba

  NI watu wachache wanaopenda kunenepa, wengi wanapenda miili ya wastani kwa kuwa  unene si mzuri. Ukiwa mnene si tu kwamba unakaribisha m...