Hukumu ya kufungwa ofisa wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Proches Kavishe aliyeshirikiana na polisi kukamata malori mawili na wafanyabiashara waliokuwa wakisafirisha bidhaa zao kutoka Kenya kuelekea Mwanza, kumefichua jinsi watumishi wa mamlaka hizo nyeti wavyochangia kuua biashara nchini.
Uonevu wa maofisa wa TRA na polisi ulioibuliwa katika kesi hiyo unaweza kuwa ni sehemu ndogo tu manyanyaso wanayopata wafanyabiashara pindi wanapoangukia kwenye mikono watumishi wala rushwa.
Ushahidi wa kushitua jinsi ofisa huyo wa TRA na askari wawili walivyokamata malori hayo na kuwalazimisha wafanyabiashara watoe rushwa ya Sh40 milioni ili waachiwe umemsikitisha Jaji wa Mahakama Kuu ambaye ametengua uamuzi wa Mahakama ya Wilaya ya Musoma iliyomwamuru ofisa wa TRA kulipa faini ya Sh500,000 na kumpa kifungo cha miaka mitano.
Jaji Zephrine Galeba ameeleza kushangazwa kwake na hakimu aliyeamuru mshtakiwa alipe faini ya Sh500,000 kwa unyanyasaji na kumwachia huru polisi aliyeshitakiwa naye licha ya kuwepo ushahidi wa kutosha dhidi yao.
Rushwa
Ilikuwa Aprili mosi, 2018 wakati wafanyabiashara wa mjini Mwanza, John Zephania na Alphonse Magesa walipokuwa wakisafiri kutoka Kenya na malori mawili yaliyosheheni bidhaa kwa ajili ya biashara Soko Kuu la Mwanza
Walipofika mpaka wa Tanzania na Kenya wa Sirari, wafanyabiashara hao na malori yao yalikaguliwa na maofisa ya forodha pamoja na wale wa uhamiaji waliwaruhusu kuendelea na safari baada ya kuridhika walifuata taratibu zote.
Hata hivyo, kilichogeuka kwa siku mbili za machungu kwa wafanyabiashara hao kilianza pale walipofika Mto Mara kwenye kizuizi cha barabarani eneo la Kirumi majira ya saa tatu na nusu usiku.
Hapo, ofisa mmoja wa TRA, Proches Kavishe na askari polisi Idrisa Majamba na Zakayo Mngulu waliokuwa wakitumia gari binafsi waliyasimamisha malori yale na kuwaamuru wayapaki pembeni mwa barabara.
Waliwafuata wafanyabiashara wale na baada ya mahojiano mafupi waliwataka watoe rushwa na Sh40 milioni ili wawaruhusu kuendelea na safari. Wafanyabiashara hao walikataa na kutumia zaidi ya saa mbili wakivutana na maofisa hao kabla ya kuamriwa kupanda kwenye magari yao na kuongozana nao kwenda Musoma mjini.
Wakiwa njiani, suala hilo likachukua sura mpya baada ya maofisa hao watatu kuamuru malori yasimame na kupaki katika kituo cha mafuta cha Lake Oil eneo la Bweri pembeni kidogo ya mji wa Musoma. Wafanyabiashara hao na malori walikabidhiwa kwa walinzi wa kituo hicho cha mafuta.
Maofisa wale wakawanyang’anya simu zao za mkononi na kuwaelekeza walinzi wa kituo kile cha mafuta kutowaruhusu kutoka katika eneo hilo.
Wakiwa wamechanganyikiwa, wafanyabiashara hao ‘mateka’ walibaki eneo hilo wakigoma kutoa rushwa hadi siku ya pili asubuhi pale ‘watesi’ wao waliporudi tena, zamu hii wakitaka Sh15 milioni. Hiyo haikusaidia, wafanyabiashara walishikilia msimamo wao wa kutotoa rushwa.
Rushwa ndani ya rushwa
Muda ulipozidi kwenda, mmoja wa askari hao Mngulu, aliwafuata tena wafanyabiashara wale na kuwataka wampe Sh400,000 ili aende kuwashawishi wenzake kukubali kupokea Sh10 milioni tu.
Kwa kuwa walikuwa wamechoka huku wakiwa na hofu ya kupoteza biashara zao, wafanyabiashara hao walilainika na kukubali kulipa Sh10 milioni ili waachiwe.
Kikabaki kikwazo kimoja, hata hivyo wafanyabiashara hawakuwa na pesa taslimu kwa hiyo malori yao hayawezi kuachiwa hadi pesa zilizotakiwa zipatikane.
Mipango ya kutuma pesa hizo kutoka Mwanza ilifanywa kwa uratibu wa ofisa wa TRA Kavishe ambaye alimpatia John Werema namba ya wakala wa M-Pesa aliyeko Musoma na pesa hizo zingetumwa kwake kutokea Mwanza.
Kufikia mchana mambo yote yalikuwa yamekamilika na malori yale yaliruhusiwa kuendelea na safari. Wakiwa na uchungu wa ‘kuporwa’ pesa zao, wafanyabiashara wale hawakupoteza muda na kwenda katika ofisi za Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) na kuomba uchunguzi ufanyike.
Adhabu ndogo
Katika uchunguzi wa Takukuru, ofisa wa TRA Kavishe na askari mmoja aliyeshirikiana naye walikamatwa na kushitakiwa katika Mahakama ya Wilaya ya Musoma kwa kujihusisha na rushwa. Wakati huo askari Mngulu alikuwa ametoweka na kusababisha kesi dhidi yake ifutwe.
Baada ya kusikilizwa ushahidi, Kavishe alitiwa hatiani kwa kupokea rushwa ya Sh10 na kuamriwa alipe faini ya Sh500,000 au kwenda jela miaka mitatu endapo angeshindwa kupipa kiasi hicho. Pia, aliamriwa arudishe zile Sh10 milioni Takukuru ili zirudishwe kwa wafanyabiashara.
Mahakama hiyo ilimwachia huru askari mwingine Majamba kwa madai ya kukosekana ushahidi wa kumtia hatiani.
Rufaa yageuka machungu
Kama Kavishe angejua rufaa aliyokata Mahakama Kuu kupinga kutiwa hatiani na kulipa faini ingegeuka balaa, pengine, asingethubutu kufanya hivyo.
Katika rufaa yake, Kavishe kupitia wakili wake Alhaj Majogoro aliiomba Mahakama kutengua hukumu iliyomtia hatiani na amri ya kulipa faini akidai kuwa upande wa mashtaka ulishindwa kuthibitisha kosa dhidi yake.
Alidai hakukuwa na ushahidi kuonyesha kuwa walalamikaji walimtambua na kwamba ndiye aliyezuia malori yasiendelee na safari.
Jaji asikitishwa
Kavishe hakuamini macho na masikio yake pale Jaji Zephrine Galeba alipoikataa rufaa yake badala yake kuamuru aende jela miaka mitano bila mbadala wa faini.
Jaji Galeba alienda mbali na kuamuru mrufani huyo alipe faini ya Sh1 milioni badala ya Sh500,000 alizoamliwa kulipa na mahakama ya wilaya.
Ushahidi dhaifu
Katika Mahakama ya Wilaya ya Musoma, Kavishe aliachiwa kwa kosa la kuomba rushwa ya Sh40 milioni lakini akatiwa hatiani kwa kosa la kupokea rushwa ya Sh10 milioni.
Kwa mujibu wa Mahakama, Kavishe hakutambuliwa na walalamikaji kuwa ndiye kati ya wale watatu aliyeomba Sh40 milioni kwa kuwa usiku ulikuwa umekwishaingia na kulikuwa na giza.
Kitendo cha Mahakama kukubali hoja kuwa Kavishe hakuwa ametambuliwa kimeonyesha wazi kutokumfurahisha Jaji Galeba.
Hata hivyo, Jaji Galela alianza kwa kuibua ushahidi ulioko kwenye rekodi za kesi hiyo unaelezea jinsi mmoja wa wafanyabiashara wale Werema aliitwa na maofisa wale ndani ya gari lao na kutaka nyaraka za mizigo waliyopakia na jinsi walivyobishana kwa muda mrefu kuhusu rushwa ya Sh40 milioni.
Jaji pia alionyesha jinsi Kavishe na askari wale walivyowapeleka wafanyabiashara katika Kituo cha Mafuta cha Lake Oil na walivyowanyang’anya simu zao za mkononi.
Akaonyesha pia jinsi Kavishe alivyompa Werema namba ya M-Pesa kwa ajili ya kutuma pesa, akisema yote hayo hayakutokea kwenya giza.
“Katika mazingira hayo, Mahakama ya Wilaya inaweza kuamua walalamikaji hawakumtambua mrufani lakini hiyo haikuwa sawa unapotazama ushahidi. Mrufani alitambuliwa na walalamikaji wote,” alisema Jaji Galeba.
Adhabu iliyopindishwa
Baada ya kutiwa hatiani, Kavishe kupitia wakili wake aliiomba Mahakama impunguzie adhabu kwa madai kuwa alikuwa bado kijana mdogo na amefanya kosa hilo kwa mara ya kwanza.
Mahakama ilikubaliana naye na kumpa adhabu ya kulipa faini ya Sh500,000 au kwenda jela miaka mitatu endapo angeshindwa kulipa.
“Hii si namna Mahakama zinatakiwa kuamua kesi za rushwa zilizothibitishwa zinazowahuru watumishi wa umma,” alisema Jaji Galeba na kuendelea kuhoji: “Ugumu hapa ni kwamba; ni katika umri gani Mahakama ilitaka mrufani awe ameufikia ili iweze kutoa adhabu stahiki?
Kigezo kingine, Mahakama ilichotumia kumpa Kavishe adhabu ndogo kilitokana na hoja kwamba hajawahi kuhusishwa na kosa la jinai kabla ya hapo.
“Ni mara ngapi Mahakama ilitaka mrufani atende kosa la jinai ili itoe adhabua anayostahili? alihoji jaji Galeba.
“Rushwa imekuwa na kugeuka jinamizi katika jamii yetu. Mahakama lazima zikatae kutoa adhabu nyepesi. Lazima zitoe adhabu kubwa kadiri inavyowezekana mtu anapotiwa hatiani kwa kosa la rushwa,” alisema.

No comments:
Post a Comment