Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Innocent Bashungwa atawaongoza mamia ya waombolezaji kuaga mwili wa aliyekuwa Katibu Mtendaji Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA), Godfrey Mngereza, aliyefariki Desemba 24, 2020 katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma alipokuwa anapatiwa matibabu.
Kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa na Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa kushirikiana na BASATA na familia mwili wa marehemu Mngereza utawasili viwanja vya Karimujee jijini Dar es salaam leo Jumanne Desemba 29, 2020 saa 3:20 asubuhi.
Mara baada ya mwili wa marehemu kuwasili katika viwanja hivyo, pamoja na taratibu nyingine za mazishi, kutakuwa na ibada fupi ya kumuombea, salamu za rambirambi pamoja na nyimbo maalum kutoka kwa wasanii na vikundi vya sanaa watakaoimba nyimbo za maombollezo kumsindikiza kiongozi huyo.
Pamoja na Bashungwa, watakuwempo pia viongozi mbalimbali wa Serikali, familia, watumishi wa Wizara na taasisi ya BASATA, wasanii, wadau wa tasnia ya sanaa, ndugu, jamaa, marafiki na baadaye safari ya kuelekea Suji wilaya ya Same mkoa wa Kilimanjaro itaanza ambapo mwili wa marehemu Mngereza utazikwa Jumatano, Desemba 30,2020.

No comments:
Post a Comment