Na Omary Mngindo, Bagamoyo
CHAMA Cha Mpira wa Miguu Wilaya ya Bagamoyo Mkoa wa Pwani (BFA), mwishoni mwa wiki kimepata viongozi wake wataokiongoza chama hicho kwa kipindi cha miaka minne ijayo.
Uchaguzi huo uliofanyika kwenye ukumbi wa Eagle chini ya Msimamizi Hafidhi Kanyamale, akisaidiwa na wajumbe wawili wanaotokea Jimbo la Chalinze Said Mkomwa na Miraji Pazi, wajumbe wapatao 73 wameshiriki zoezi hilo, huku Olnjure Marigwa akichaguliwa Mwenyekiti.
Katika kinyang'anyiro hicho kilichokuwa na nafasi za Mwenyekiti, Makamu, Katibu na Msaidizi wake, Mhazini, Mjumbe kuwakilisha Wilaya kwenda Mkoa na Mjumbe wa kuwakilisha Vilabu, hata hivyo Mjumbe kuwakilisha vilabu nafasi hiyo haijapata mwakilishi.
Mwakilishi wa vilabu Wilaya iliyokuwa inawania na mgombea mmoja Mohamed Mbaruku, kati ya kura 73 zilizopigwa amepata kura za ndio 18 tu, huku 47 zikisema hapana, wakati mbili zikiharibika hivyo nafasi hiyo kukosa mwakilishi.
Marigwa ameibuka kinara kwa kura 53 dhidi ya mgombea mwenzake James Manyama 13, Makamu Mwenyekiti Abdul Pyalla hakuwa na mpinzani akipata kura 55, huku Katibu Mkuu akishinda Salum Kanema kura 60 nae hakuwa na mpinzani, baada ya aliyetaka kutetea Hussein Kipindura kukatiwa rufaa.
Katibu Msaidizi amechaguliwa Azizi Mwashambwa kwa kura 61, Mhazini Ibrahimu Gama kura 56 akimshinda Ibrahimu Huruka, Mjumbe kuwakilisha Wilaya kwenda Mkoa Ramadhani Rukanga aliyemshinda Kitoro Jonas.
Akizungumza baada ya matokeo hayo, Hafidhi alisema kuwa zoezi hilo halikushirikisha Wajumbe wa Kamati ya Itendaji, hivyo amewaagiza viongozi hao kujipanga kwa ajili ya kukamilisha safu hiyo, sanjali na nafasi ya Mwakilishi wa vilabu wilaya.
"Kwanza niwashukuru wajumbe kwa utulivu mkubwa katika kukamilisha zoezi letu la uchaguzi, niwaombe viongozi mjipange ili kujazia nafasi zilizokuwa wazi kianzia Wajumbe Kamati ya Utendaji na Mwakilishi wa vilabu wilaya," alisema Kanyamale.
Ofisa Utamaduni wilaya Vedastus Mziba amewataka viongozi wa vilabu na wadau wa mchezo huo wawaunge mkono ili kwa umoja wao waweze kufanikisha kiu ya wana-Bagamoyo katika medani hiyo yenye mashabiki wengi nchini na duniani kwa ujumla.

No comments:
Post a Comment