Search This Blog

Monday, August 3, 2020

RITA YATOA USHAURI KWA JAMII KUZINGATIA USAJILI WA VYETI VYA WATOTO KISHERIA WAKATI WA KUASILI

Na Mwandishi Wetu,Michuzi TV

WAKALA wa Usajili Ufilisi na Udhamini (RITA) umetoa ushauri kwa jamii kuzingatia kusajili cheti /vyeti  vya watoto kisheria pale wanapotaka kuasili mtoto au watoto.

Kwa mujibu wa taarifa ya RITA iliyoitoa kwa vyombo vya habari leo Agosti 3,2020 imesema inafahamika katika jamii ya kitanzania wapo watoto wanaokulia katika vituo vya kulelea watoto yatima ama kwasababu ya wazazi kufariki, hawajulikani walipo au hawana uwezo wa kuwapatia matunzo.

Vivyo hivyo wapo watu wazima ambao wanashauku ya kuwa na mtoto hata wa kuasili na hiyo ni kwasababu ya pengine kutojaaliwa kuwa na watoto wa kuwazaa.

Imesema Sheria ya mtoto Na. 21 ya mwaka 2009 imeweka utaratibu Kisheria  ili kuweza kusaidia watu wanaotaka kuasili mtoto/watoto kisheria. Kuasili mtoto maana yake ni utaratibu wa kumpatia mtoto aliyekosa mazingira ya kifamilia kupata matunzo ya kudumu ya kifamilia.

"Jumla ya vyeti 863 vimesajiliwa na Wakala wa Usajili Ufilisi na Udhamini (RITA) kutokana na watu mbalimbali kuleta maombi yao ya kutaka  kusajili cheti cha kuasili mtoto. 

"Ili kuweza kusajili cheti cha kuasili mtoto kisheria katika ofisi za RITA makao makuu muombaji anapaswa kuwasilisha nakala ya uamuzi kutoka  mahakama kuu na pia cheti cha kuzaliwa cha mtoto anayeasiliwa,"imesema RITA kwenye taarifa hiyo.

Imesisitiza ni  muhimu jamii kujua umuhimu wa kusajili cheti cha kuasili mtoto kwani kitasaidia katika kumpatia mahitaji yake ya msingi kama vile elimu,chakula,malazi na masuala ya afya kwa ujumla kama ambavyo watoto wengine wanapata katika jamii. 

"Moja ya haki za mtoto ni kulindwa jambo ambalo watoto wasiokuwa na wazazi wamekuwa wakiteseka kwa kuishi mazingira ambayo si rafiki, mazingira ambayo hayana ulinzi na kupelekea kufanyiwa vitendo viovu na watu wasiokuwa na maadili kama vile kubakwa na kunyanyaswa kijinsia pamoja na mambo mengine.

"Hatahivyo iwapo mtu atasajili cheti cha kuasili sheria itamchukulia kuwa ni sawa na mzazi wa mtoto husika hivyo itasaidia pia kupunguza wimbi la watoto wa mitaani linalokuwa kila kukicha. Hii itasaidia pia kwa Serikali kuweza kupata takwimu sahihi ya wananchi wake katika kupanga mipango mbalimbali ya kimaendeleo katika jamii yake kama vile elimu,"imesema.

Imeongeza kwamba Wakala umetoa ushauri kwa mtu aliyekidhi vigezo vya kuasili mtoto kwa mujibu wa sheria  kuweza kuzingatia kusajili cheti hicho katika Ofiza  za RITA makao makuu Dar Es Salaam  mara baada ya kupata nakala ya uamuzi kutoka mahakama kuu.

RITA inashiriki katika maonesho ya Nanenane yanayofanyika kitaifa mkoani Simiyu na huduma zinazotolewa ni Elimu kwa umma kuhusu kuasili watoto, Usajili wa vizazi na vifo, Wosia na mirathi, Ndoa na talaka pamoja na udhamini. Wananchi wanakaribishwa kutembelea banda la RITA namba 94 lililopo upande wa geti la kuingilia karibu na banda la NIDA ili kufaidika na huduma hizo.
 Afisa Usajili Msaidizi Bi. Adressa Magwira akikabidhi vipeperushi kuhusu huduma za RITA kwa aliyekuwa Katibu Tawala mkoa Mhe. Jumanne Sagini alipotembelea banda la RITA katika maonesho ya Nanenane viwanja vya Nyakabindi mkoani Simiyu.
Aliyekuwa Katibu Tawala mkoa wa Simiyu Mhe. Jumanne Sagini(kushoto) akiweka saini yake katika kitabu cha wageni alipotembelea banda la RITA.
Aliyekuwa Katibu Tawala mkoa wa Simiyu Mhe.Jumanne Sagini akipata maelezo kuhusu huduma za RITA kutoka kwa Afisa Usajili Msaidizi, Bw. William Mgasha.


No comments:

Post a Comment

Punguza kilo tano kwa siku saba

  NI watu wachache wanaopenda kunenepa, wengi wanapenda miili ya wastani kwa kuwa  unene si mzuri. Ukiwa mnene si tu kwamba unakaribisha m...