Msemaji wa Majeshi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameonya kuwa, iwapo utawala wa Kizayuni wa Israel utaendelea kufanya shari na maovu yake, basi utakabiliwa na pigo kubwa kutoka kwa mrengo wa muqawama na Iran.
Brigedia Jenerali Abolfazl Shekarchi alitoa indhari hiyo jana Alkhamisi na kusisitiza kuwa, Israel itashuhudia izza na nguvu za Iran ikiendelea kufanya vitendo vyake vya shari na ovu.
Amewaonya watawala wa Tel Aviv wasithubutu kuupa majaribu na mtihani uwezo mkubwa wa Jamhuri ya Kiislamu na mrengo wa muqawama katika eneo la Asia Magharibi, kwani utawala huo pandikizi utakabiliwa na kipigo kikali.
Matamshi ya Msemaji wa Majeshi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni jibu kwa madai yasiyo na msingi ya utawala wa Kizayuni ya eti umeshambulia maeneo kadhaa ya washauri wa kijeshi wa Iran nchini Syria.
Brigedia Jenerali Abolfazl Shekarchi amekumbusha kuwa, katika kipindi cha miaka tisa ya uwepo wa washauri wa kijeshi wa Iran nchini Syria kihalali kwa ajili ya kukabiliana na kundi la kigaidi la Daesh (ISIS), askari wanane wa Jamhuri ya Kiislamu wameuawa shahidi katika mashambulizi ya mabomu ya jeshi la utawala haramu wa Israel.
Mgogoro nchini Syria ulianza mwaka 2011 kwa hujuma na mashambulio makali ya makundi ya kigaidi yanayofadhiliwa na Saudi Arabia, Marekani na waitifaki wao kwa lengo la kubadilisha mlingano wa nguvu katika eneo la magharibi mwa Asia kwa maslahi ya utawala wa Kizayuni wa Israel
Hata hivyo kwa msaada wa washauri wa kijeshi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na uungaji mkono wa Russia, jeshi la Syria limefanikiwa kulisambaratisha kundi la kigaidi la Daesh nchini humo.


No comments:
Post a Comment