Search This Blog

Tuesday, July 21, 2020

Iran inataka kuona Iraq yenye izza na huru, Marekani ni adui


Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa Iran inataka kuona Iraq yenye izza sambamba na kulindwa ardhi yote ya nchi hiyo na mshikamano wa ndani; kinume chake Marekani ni adui halisi na haitaki kuwepo Iraq inayojitawala, yenye nguvu na yenye serikali iliyochaguliwa na waliowengi.
Ayatullah Ali Khamenei aliyasema hayo jana jioni katika mazungumzo yake na Waziri Mkuu wa Iraq, Mustafa al Kadhimi aliyeko ziarani hapa nchini. Ameashiria upinzani wa Iran dhidi ya hatua ya aina yoyote inayodhoofisha serikali ya Iraq na kusema: Jambo linalopewa umuhimu mkubwa sana na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika uhusiano wa pande mbili ni maslahi, amani, izza, nguvu ya kieneo na hali bora ya Iraq. 
Ayatullah Khamenei amesema mtazamo wa Wamarekani kuhusiana na Iraq unakabiliana na kutofautiana kikamilifu na wa Iran na kuongeza kuwa, Iran haiingilii uhusiano wa Iraq na Marekani lakini inatarajia kuwa, marafiki wa Iraq wataijua vyema Marekani na kuelewa kwamba, kuwepo Wamarekani katika nchi yoyote huwa chanzo na sababu ya ufisadi, uharibifu na uovu.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amekumbusha kwamba: Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inatarajia kuwa uamuzi wa Serikali, taifa na Bunge la Iraq wa kuwafukuzwa Wamarekani nchini humo utatekelezwa kwa sababu kuwepo kwao ni chanzo cha ukosefu wa amani.
Amesema kuwa mauaji ya kigaidi yaliyofanywa na Marekani dhidi ya Luteni Jenerali Qassem Soleimani na Shahidi Abu Mahdi al Muhandis ni mfano wa wazi wa matokeo ya kuwepo Wamarekani nchini Iraq na kuongeza kuwa: Jamhuri ya Kiislamu kamwe haitasahau suala hilo na hapana shaka kuwa italipiza kwa kutoa kipigo kwa Wamarekani. 


Ayatullah Ali Khamenei amesema kuwa, suala la kuimarishwa uhusiano baina ya Iran na Iraq linapingwa na baadhi ya nchi zikiongozwa na Marekani lakini haipaswi kabisa kuiogopa Marekani kwa sababu haiwezi kufanya lolote. 
Ayatullah Khamenei amesema kuwepo kwa kiongozi mkuu wa kidini wa Iraq Ayatullah Ali Sistani ni neema kubwa kwa Iraq na kuongeza kuwa, harakati ya wananchi ya al Hashdu al Shaabi ni neema nyingine kubwa nchini Iraq ambayo inapaswa kulindwa. 
Kwa upande wake Waziri Mkuu wa Iraq amesema kuwa amefurahishwa sana kwa kukutana na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu na ameshukuru misimamo na hiyama ya Iran kwa nchi yake katika vipindi na nyakati mbalimbali hususan wakati wa vita vya kukabiliana na kundi la kigaidi la Daesh na makundi ya kitakfiri. Mustafa al Kadhimi amesema kuwa, Wairaqi kamwe hawatasahau himaya na misaada ya Iran na kuongeza kuwa, ukweli ni kwamba damu za Wairaqi na Wairani zilichanganyika katika vita dhidi ya makundi ya kitakfiri.
Al Kadhimi amesisitiza kuwa, uhusiano wa Iran na Iraq ni mkubwa, wa kihistoria, kiutamaduni na kidini unaofungamanishwa pamoja na mapenzi ya mataifa hayo mawili kwa Mtume (saw) na Ahlibaiti zake watoharifu.
Waziri Mkuu wa Iraq amesema kuwa, miongozo na nasaha za Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ni mithili ya funguo za kutatua matatizo.     


No comments:

Post a Comment

Punguza kilo tano kwa siku saba

  NI watu wachache wanaopenda kunenepa, wengi wanapenda miili ya wastani kwa kuwa  unene si mzuri. Ukiwa mnene si tu kwamba unakaribisha m...