
YANGA ina siku nne ngumu ndani ya Uwanja wa Taifa ambazo zitaamua hatma yao ya nafasi ya pili msimu huu. Kesho Jumapili wanacheza dhidi ya Azam ndani ya uwanja huo na Jumatano watarudi tena hapo hapo kuwavaa Namungo.
Ni timu mbili ngumu ambazo zinawania nafasi ya pili ya tatu sambamba na Yanga ambayo kocha wake, Luc Eymael amesisitiza kwamba anahitaji angalau nafasi ya pili tu kwavile ubingwa umeng’ang’aniwa tayari na Mnyama Simba.
Kama Yanga itapoteza mechi hizo au kupata sare bado itakuwa imejiweka kwenye mazingira magumu baada ya sare ya mwisho dhidi ya JKT Tanzania mjini Dodoma.
Matokeo hayo yaliifanya Yanga isalie katika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa Ligi ikiwa na pointi 55 ambazo ni 17 nyuma ya vinara, Simba wenye pointi 72.
Yanga watakuwa wanalikosa taji hilo kwa mara ya tatu mfululizo ikiwa ni kwa mara ya kwanza tangu ilipotokea hivyo mwaka 1993, 1994, 1995.
NAMUNGO, AZAM TISHIO
Hizi ndio timu mbili zilizobeba heshima ya Yanga. Kwa nafasi ya pili, Yanga ina kibarua kizito mbele ya Azam FC ambayo iko juu yao kwa tofauti ya pointi mbili.
Yanga inawakabili Azam kesho Jumapili, ikiwa ni karata muhimu ya Wanajangwani kuweka hai angalau matumaini ya kumaliza katika nafasi ya pili kwani wakipoteza maana yake watatanguliwa na Azam kwa pointi tano.
Lakini wakimaliza hapo wanageukia kwa Namungo ambayo itapaswa kuhakikisha haiwapi nafasi kuwapiku kwani nao wanakuja vizuri.
Yanga iko mbele ya Namungo yenye alama 51 kwa tofauti ya pointi nne na timu hizo mbili zina mechi baina yao ambayo itafuata baada ya ile ya Yanga na Azam.
Kufanya vibaya kwa Yanga katika michezo hiyo miwili mfululizo na ikiwa Namungo itafanya vizuri, maana yake, Namungo itakuwa juu ya Yanga kwa tofauti ya pointi mbili.
MECHI SITA ZA SHOKA
Ugumu wa Yanga ni wazi kwamba unaongezwa na mechi sita (6) ambazo italazimika kupata ushindi ili kumaliza katika nafasi za juu msimu huu.
Baada ya kumalizana na Azam na Namungo, mechi nyingine ngumu ambazo Yanga itacheza kati ya tisa (9) ilizobakiza ni dhidi ya Biashara United, Kagera Sugar, Lipuli na Mtibwa Sugar ambazo zote itacheza ugenini.
Hata hivyo, ina afueni ya kuwa na mechi mbili nyumbani zinazoonekana kutokuwa na ugumu kwake ambazo ni dhidi ya Ndanda FC na Mwadui FC.
NJIA NGUMU
Matumaini makubwa kwa Yanga msimu huu ni ubingwa wa Kombe la Shirikisho la Azam ambalo bingwa wake ndio huwakilisha nchi katika Kombe la Shirikisho Afrika.
Hata hivyo, huko nako hakuonekani kuna urahisi kwa Yanga kutimiza ndoto zake kutokana na timu zilizobakia na ratiba ilivyopangwa hadi kufika hatua ya fainali.
Katika hatua ya robo fainali, Yanga imepangwa kukutana na Kagera Sugar iliyowafunga mabao 3-0 katika mchezo wa mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu msimu huu.
Ikiwa itaitoa Kagera Sugar, itakutana na mshindi baina ya Simba na Azam katika mchezo wa nusu fainali
MIKAKATI YA KOCHA
Kocha wa Yanga, Luc Eymael alisema; “Sio jambo rahisi lakini naamini vijana watafanya kazi nzuri katika mechi zilizobakia. Changamoto kubwa ni viwanja ambavyo vingi havina eneo zuri la kuchezea.”
Amesisitiza kwamba wanahitaji kushinda mechi ngumu za nyumbani dhidi ya Azam na Namungo kwa namna yoyote ili kupunguza makali ya washindani wao na wachezaji wake amewasisitiza hilo.
Mkurugenzi wa Uwekezaji wa GSM inayoidhamini Yanga, Injinia Hersi Said hivi karibuni alisema kuwa watatoa motisha nzuri kwa wachezaji ili wafanye vyema kwenye Ligi na watwae Kombe la Shirikisho.
“Hakuna mdhamini anayetaka kusikia matokeo mabaya kwa timu anayofanya nayo kazi lakini narudia tena sisi GSM ni familia ya Yanga, ndio maana tumeona tuwape ahadi nzuri vijana,” alisema Hersi.
No comments:
Post a Comment