Search This Blog

Thursday, June 4, 2020

Hao Simba duh! Azam, Yanga waachwa parefu

By THOBIAS SEBASTIAN

KAMA anachokitaka Kocha wa Simba, Mbelgiji Sven Vandenbroeck kikifanikiwa wataandika rekodi ya aina yake kabla ya kumalizika kwa msimu huu.

Anachotaka afanyiwe huko mazoezini na viongozi, Yanga na Azam hawajawahi kufikiria.

Kocha huyo amewapa masharti mabosi wake ambayo anataka yatekelezwe kabla ya msimu huu kumalizika ili kuhakikisha mambo yananoga zaidi na yanakwenda kisayansi ndani ya kikosi hicho.

Anataka kikosi hicho chenye mipira 51 iongezwe mingine 49, ili kufikisha jumla ya mipira 100 kwani kuna mazoezi mengi ya kutumia mipira amepanga kuyafanya. Mpira mmoja thamani yake ni kuanzia Sh120,000.

Tathmini ya Mwanaspoti kwenye mazoezi ya Yanga na Azam kwa sasa imebaini kwamba Azam wanatumia mipira 25 mazoezini sawa na Yanga na hata zikiongezeka programu za pembeni haizidi 30.

Pia Sven ametaka tena aongezewe vifaa vingine vya mazoezi kama yale maputo magumu, koni, viunzi, midoli ya watu ya plastiki ambayo huchomekwa uwanjani kama watu wa bandia, fimbo ndefu na fupi za plastiki na vifaa vingine vingi kwani alivyo navyo sasa havimtoshi anataka kufanya mambo zaidi.

Advertisement

Mbali ya hivyo, Sven ametaka kila mchezaji aongezewe jezi za kufanyia mazoezi na zile ambazo atazitumia katika mechi.

Mwanaspoti linafahamu katika jambo hilo la Sven kutaka hivyo vifaa vya mazoezi tayari meneja wa kikosi hicho, Patrick Rweyemamua na mtunza vifaa vya timu, Khamis Mtambo wamefanya kikao na ofisa mtendaji, Senzo Mazingisa juu ya mahitaji hayo na tayari wameanza harakati ya kwenda kuvitafuta.

Mmoja wa viongozi wa ufundi wa Simba alisema kwamba kocha amewaambia kuwa anataka kuongeza vifaa hivyo ili kuwa na wigo mpana wa kutekeleza majukumu yake na kuiimarisha Simba kiufundi.

Ukiachana na jambo hilo, Sven amezungumzia ratiba ya ligi ambayo imetoka juzi kuwa ni nzuri kwao na inaweza kuwarahisishia mbio zao za ubingwa.

Sven alisema anafahamu watakuwa wanacheza mechi kila baada ya siku tatu ila uzuri wake katika michezo kumi ambayo wamebaki nayo wanahitaji kushinda mitano ili kubeba ubingwa, na wataanza kucheza mbili katika uwanja wa nyumbani.

Anasema kwa ambavyo wachezaji wamerudi katika ufiti na hali ya ushindani anaona mechi mbili watakazocheza nyumbani watakuwa na uhakika wa kupata pointi tatu.

“Nafahamu katika mpira lolote linaweza kutokea kutokana na (wapinzani wetu) ambao tunakutana nao muda huu wanajiandaa pia,” anasema.

“Wachezaji wangu wamerudi katika hali nzuri ya kushindana, inaonekana walikuwa wanafanyia kazi kweli zile programu ambazo niliwaachia wakati ligi ikiwa imesimama.

“Kwa maana hiyo tumeanza na mazoezi ya nguvu ili kuwa katika levo sawa ya kushindana na baada ya hapo tunaanza mazoezi ya mbinu ambayo ndio yatakuwa mengi mpaka kuanza kwa ligi.”

Aliongeza kuwa: “Nadhani maendeleo katika maandalizi yetu haya ni mazuri kwani kila siku wachezaji wanabadilika katika ufiti wa miili yao na mbinu ambazo tunawapatia wanazielewa vizuri, kwa maana hiyo kama benchi la ufundi tunaona mwanga wa kile ambacho tunakwenda kukutana nacho na tunaona tunaweza kufikia malengo yetu.

“Kwa maana hiyo muda ambao tumeupata kufanya maandalizi kwetu umekuwa mzuri, ingawa tungepata zaidi ya hapo ingekuwa bora zaidi, yote kwa yote ratiba ya ligi ni nzuri kwetu, maandalizi hasa yale ya kiufundi yanakwenda vizuri na kilichobaki ni wachezaji kukipeleka uwanjani kile ambacho tunawapatia huku mazoezini.”

Let's block ads! (Why?)

No comments:

Post a Comment

Punguza kilo tano kwa siku saba

  NI watu wachache wanaopenda kunenepa, wengi wanapenda miili ya wastani kwa kuwa  unene si mzuri. Ukiwa mnene si tu kwamba unakaribisha m...