
Baada ya kukosa mchezo uliopita dhidi ya Mwadui FC, kiungo wa Yanga, Feisal Salum 'Fei Toto' huenda akarejea katika mchezo wa kesho Jumatano dhidi ya JKT Tanzania utakaochezwa kwenye Uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma.
Katika mazoezi ya mwisho ambayo Yanga walifanya jana Jumanne, kwenye uwanja wa Jamhuri Dodoma, Fei Toto alikuwa sehemu ya kikosi ambacho kinaweza kuanza katika mchezo wa kesho dhidi ya JKT Tanzania.
Kocha wa Yanga, Luc Eymael alisema kiungo huyo amefanya mazoezi vizuri na kuonesha ushawishi wa kupewa nafasi kwenye kikosi cha kwanza ambacho kitacheza mechi ngumu kesho.
Eymael alisema alikuwa anamfatilia Fei Toto tangu alipofika kambini siku moja kabla ya kucheza na Mwadui, na alionesha kutimiza vyema majukumu yake kwa nafasi ambayo anacheza.
"Awali sikuwa najua kama ana kadi tatu za njano. Nilimpanga katika kikosi cha kwanza, kabla ya kutaja kikosi hicho kwa wachezaji, ndio wasaidizi wangu wakanieleza hataweza kucheza kutokana na kutumikia adhabu hiyo kwa kukosa mchezo mmoja.
"Inaonekana kipindi ambacho ligi ilikuwa imesimama Fei Toto alikuwa anafanya mazoezi ya kutosha kulingana na programu ambayo tuliwapatia lakini hata yale mazoezi yake binafsi," alisema Eymael.
No comments:
Post a Comment