
MADRID, HISPANIA. SAMUEL Eto’o kwa mara nyingine tena amefunguka kwamba, anamkubali na kumuelewa zaidi kocha Jose Mourinho kuliko Pep Guardiola.
Nahodha huyo wa zamani wa timu ya Taifa ya Cameroon, Eto’o amepata nafasi ya kucheza chini ya makocha hao mahasimu kwa nyakati tofauti. Alicheza chini ya Guardiola kwenye kikosi cha Barcelona na kushinda mataji kibao na baadaye akakipiga chini ya Mourinho akiwa na Inter Milan na baadaye Chelsea ya England.
“Uzoefu wangu na Pep tukiwa Barcelona ulikuwa kama ambavyo ilikuwa, lakini upande wa maisha mengine haikuwa sawa. Ndivyo ambavyo hata wachezaji wengine wanavyoweza kumzungumzia kocha huyu.
“Kama Pep katika kujiandaa na mchezo hakuna kama yeye. Alivyotufundisha mwaka 2009 ilikuwa hatari na kuanzia katika namna ya kuumiliki mpira, kushambulia hakika hana mfano katika hilo.
“Kama mchezaji unaweza kujiona kama hukimbii sana kwa sababu tulikuwa tukifurahia,” alisema Eto’o na kuongeza: Jose alikuwa rafiki wa kila mtu, aliweza kucheza na saikolojia zetu vizuri.
“Ni mtu safi, ambaye ni rahisi kukweleza jambo ambalo hajafurahishwa nalo. Ni mtu bora zaidi kuwahi kukutana naye katika soka, amekuwa wa matukio, mengine ni mbinu za kimchezo, anajua kujiandaa ndani ya nje. Hakuna kama Mou.”
Akiwa na FC Barcelona, Eto’o alikuwa moto kwelikweli akishinda na mataji ya Ligi Kuu ya Hispania, La Liga, Ligi ya Mabingwa Ulaya, 2005/06 na 2008/09 wakati kwa Mourinho alibeba msimu 2009/10 wakiwa na Inter Milan.
No comments:
Post a Comment