Search This Blog

Wednesday, May 13, 2020

Taasisi ya Dkt Msuya yakabidhi vifaa vya corons kwa misikiti Wilayani Mwanga


WANANCHI wametakiwa kuvitunza na kuvithamini vifaa vya kujikinga na maambukizi ya ugonjwa wa Corona vinavyotolewa na wadau mbalimbali nchini katika kusaidia kujikinga na ugonjwa huo.

Kauli hiyo imetolewa wilayani Mwanga Mkoani Kilimanjaro na Mkurugenzi wa Taasisi ya Dk Msuya, Dk Ombeni Msuya wakati akikabidhi mashine za kisasa za kunawia mikono kwenye Misikiti na Zahanati wilayani humo.

Taasisi hiyo ya Dk Msuya imekua ikiiunga mkono serikali katika sekta mbalimbali ikiwemo pia ya Elimu na toka ugonjwa wa Corona uingie nchini imekua ikihamasisha wananchi kuchukua hatua za kujikinga na ugonjwa huo kama ambavyo serikali imekua ikisisitiza.

Dk Msuya amesema mashine hizo zitasaidia wananchi kutumia maji na sabuni kwa kukanyaga kwa miguu bila kutumia mikono jambo ambalo linapunguza pia uwepo wa maambukizi kwenye koki za bomba kwa kila mtu kuigusa.

" Lengo la misaada yetu hii ambayo pia tumegawa kwenye Taasisi za Dini ya Kikristo, Ofisi ya Mkuu wa Wilaya na maeneo mengine ni kuiunga mkono serikali yetu ambayo chini ya Rais Magufuli imechukua hatua mbalimbali za kuwakinga wananchi na ugonjwa huu.

Hivyo niwaombe wote mtakaotumia vifaa hivi tuvitunze kwani hatujui Corona itaisha lini. Lakini pia tuvitumie ipasavyo ili tuweze kuepukana na maambukizi ya ugonjwa huu," Amesema Dk Msuya.

Amebainisha kuwa mashine zilizokabidhiwa kwenye Misikiti hiyo wilayani Mwanga ni 10 na kuahidi kuendelea kushirikiana na serikali katika kuwahudumia watanzania.

Kwa upande wake Katibu wa Bakwata Wilaya ya Mwanga, Ustaadhi Iddi Mchome ameishukuru Taasisi hiyo kwani vitakua msaada kwa Waislamu na wasio waislamu katika kujikinga na Corona.

Ustaadhi Mchome amesema walikua wanakabiliwa na changamoto ya kutumia vifaa duni ambavyo kila mtu atashika mkono wakati wa kunawa lakini kupitia mashine hizo sasa zitakua msaada kwani ili unawe inabidi utumie miguu kubonyeza mashine hizo.

" Kwa niaba ya waislamu wa Wilaya ya Mwanga tunaishukuru sana Taasisi hii, mmeonesha moyo wa kizalendo sana kwetu sisi. Hatuna cha kuwalipa zaidi ya kuwaombea dua na kuvitunza vifaa hivi," Amesema Ustaadhi Mchome.


No comments:

Post a Comment

Punguza kilo tano kwa siku saba

  NI watu wachache wanaopenda kunenepa, wengi wanapenda miili ya wastani kwa kuwa  unene si mzuri. Ukiwa mnene si tu kwamba unakaribisha m...