Search This Blog

Wednesday, May 27, 2020

ROWODO yaunga mkono juhudi za serikali mapambano dhidi ya COVID-19


Na Ahmad Mmow, Lindi.

Shirika lisilo la kiserikali la maendeleo ya wanawake wa Rondo limepanga kutumia shilingi 30,000,000 kwa ajili ya utekelezaji wa  wa mradi wa ushawishi na utetezi juu ya uimarishaji wa elimu na uzingatiaji wa maelezo ya jinsi ya kujikinga na homa kali ya mapafu( COVID-19) unaosababishwa na virusi vya Corona.

Hayo yalielezwa jana mjini Mtama , na mkurugenzi wa ROWODO, Scholastica Nguli wakati wakutambulisha mradi huo utakaotekelezwa kwa miezi mitatu, (kuanzia mwezi Mei hadi Julai, mwaka 2020) katika kata nane zilizopo katika halmashauri ya Mtama, wilaya ya Lindi.

Nguli alisema ROWODO kwa ufadhili wa mfuko wa asasi za kiraia( FCS) kupitia mradi wa Mfumo wa ufuatiliaji wa matumizi ya raslimali za umma( PETS) ambao uliendelea kutekelezwa mwezi Mei, mwaka huu wa 2020 na ambao ulianza kutekelezwa  mwezi Julai, mwaka 2019 lilialikwa liandike andiko la mradi ambalo litaunga mkono jitihada za serikali za kupambana na ugonjwa huo hatari ili kufikia malengo ya mpango wa dharura.

Alisema shirika hilo na mengine takribani 150 ambayo ni wabia wa FCS  yalishindanishwa  na kuwasilisha maandiko ya mradi huo kwa FCS ambalo linafadhili. Ndipo ROWODO na mashirika mengine 19 yakashinda na kila moja limefadhiliwa kiasi hicho cha fedha kitakachotumika kutekeleza mradi huo.

Nguli alizitaja kata zitakazo fikiwa na mradi huo kuwa ni nane ambazo pia zipo kwenye mradi wa PETS ambao unaendelea kutekelezwa kwa mujibu wa maelekezo ya FCS ili iwe rahisi kuwapata wanajamii wa ngazi ya chini ambao wataendeleza shughuli za utoaji elimu. Lakini pia maeneo hayo nayo yanauhitaji wa elimu ya COVID-19  kama maeneo mengine.

" Wataalamu wa afya katika halmashauri ya Mtama pamoja na viongozi wa serikali ngazi ya wilaya watashirikishwa katika mradi huu. Hususani katika kutoa maelekezo , kusimamia, uzingatiwaji wa tahadhari na utoaji wa taarifa rasmi za kiserikali kuhusu utekelezaji wa mikakati ya serikali katika kudhibiti kuenea kwa ugonjwa huo katika maeneo mbalimbali," alisema Nguli.

Alizitaja kata zitakazofikiwa na kutekelezwa mradi huo kuwa ni Namangale, Nyengedi, Majengo, Mtama, Nyangamara, Pangatena, Nyangao na Mtua. Huku akiweka wazi kwamba kuna aina tatu za makundi yanayolengwa katika mradi huo kuwa ni jamii, taasisi za utoaji huduma, viongozi na watendaji wa halmashauri ya Mtama.

Alisema katika kundi la makundi ya kijamii watakaolengwa ni watu wenye ulemavu, wasiojiweza, wazee, wagonjwa walio majumbani, waumini wa dini mbalimbali, wafanyabiashara ndogondogo na makundi ya wasafirishaji. Lakini pia kundi la wanufaika litawahusisha wahudumu wa afya,  askari na maofisa ulinzi na usalama, hospitali, zahanati, maduka makubwa, hoteli na migahawa.

" Makundi haya yawanufaika yanahusishwa katika mradi huu kutokanana mazingira ya kazi zao na huduma wanazotoa kwa jamii ambazo muda mwingi wanalazimika kukutana na watu tofauti kwenye  maeneo yao ya kazi," alisisitiza Nguli.

Kwaupande wake mwenyekiti wa halmashauri ya Mtama, Methew Makwinya licha ya kupongeza shirika hilo na FCS kwakuunga mkono jitihada za serikali, alishauri idadi ya kata zitakazofikishwa mradi huo ziongezwe. Hasa maeneo yenye watu wengi na msongamano. Ikiwamo kata ya Kiwalala.



No comments:

Post a Comment

Punguza kilo tano kwa siku saba

  NI watu wachache wanaopenda kunenepa, wengi wanapenda miili ya wastani kwa kuwa  unene si mzuri. Ukiwa mnene si tu kwamba unakaribisha m...