Search This Blog

Thursday, May 14, 2020

Burundi yawatimua nchini humo maafisa wa WHO wakati huu wa corona



Serikali ya Burundi imemfukuza nchini humo Mkuu wa Shirika la Afya Duniani (WHO) nchini humo na maafisa watatu wa timu yake waliokuwa wakifuatilia mwenendo wa mlipuko wa ugonjwa wa Covid-19 (corona) katika nchi hiyo.

Wizara ya Mambo ya Nje ya Burundi imeiandikia barua ofisi kuu ya WHO barani Afrika, ikitaka iwaondoe maafisa wake hao nchini humo kufikia leo Ijumaa.

Maafisa hao wa WHO waliotimuliwa ni pamoja na Mwakilishi Mkazi wa WHO nchini Burundi, Dakta Walter Kazadi Mulombo, Dakta Jean Pierre Mulunda Nkata, mshirikishi wa mlipuko wa corona wa WHO, Dakta Ruhana Mirindi Bisimwa, Mkuu wa Magonjwa ya Kuambukiza na Profesa Daniel Tarzy, mtaalamu wa maabara ya kupima virusi vya corona wa shirika hilo la afya duniani.

Afisa mmoja wa Wizara ya Afya ya Burundi ambaye hakutaka kutaja jina lake ameliambia shirika la habari la AFP kuwa, maafisa hao wa WHO wametimuliwa kwa kukosoa namna wizara hiyo inavyolishughulikia janga la corona.

John Nkengasong, Mkuu wa Kituo cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa cha Afrika (CDC) ameeleza kusikitishwa kwake na hatua hiyo ya kutimuliwa maafisa wa WHO na kusema kuwa, uamuzi huo umechukuliwa wakati huu nyeti ambapo ushirikiano unahitajika ili kuweza kuushinda ugonjwa huo barani humo.


WHO na CDC-Afrika zilionyesha wasiwasi wao wa kuendelea kufanyika mikutano ya kampeni za uchaguzi mkuu ujao nchini humo katika kipindi hiki cha janga la ugonjwa wa Covid-19 (corona). Kwa mujibu wa takwimu za serikali, nchi hiyo yenye jamii ya watu milioni 11 imerekodi kesi 27 tu za watu walioambukizwa virusi vya corona hadi sasa, huku mtu mmoja akiaga dunia kwa ugonjwa wa Covid-19.

Uchaguzi wa urais, bunge na madiwani nchini Burundi unatazamiwa kufanyika tarehe 20 ya mwezi huu wa Mei.

No comments:

Post a Comment

Punguza kilo tano kwa siku saba

  NI watu wachache wanaopenda kunenepa, wengi wanapenda miili ya wastani kwa kuwa  unene si mzuri. Ukiwa mnene si tu kwamba unakaribisha m...