
TUKIWA bado tunaendelea katika tahadhari ya juu ili kujikinga na ugonjwa wa corona au COVID-19 si vibaya kuendelea kupeana ufahamu kuhusu utimamu wa mwili na mazoezi kwa wanamichezo au wafanya mazoezi wa kawaida.
Kutokana na tishio la corona hivi sasa ni kawaida kufanya mazoezi ya kujitenga au kufanya mazoezi ndani ya nyumba kwa lengo la kujihami na mikusanyiko au misongamano ambayo ni moja ya njia ya kuenea kwa virusi vya corona.
Mfanya mazoezi ya kawaida huwa na lengo la kujenga mwili wenye afya njema wakati yule mwanamichezo, ambaye michezo ni ajira huwa na lengo la kuwa na utimamu wa mwili, kulinda na kukuza kiwango chake.
Tukiwa tunaendelea kujikinga na ugonjwa huu ni vizuri kujua kuwa mafanikio kwa mfanya mazoezi au mwanamichezo huletwa na vitu vinne ambavyo ni kula, kulala au kupumzika, mazoezi na nidhamu.
Vitu hivi vinne hutegemeana kutoka kimoja kwenda kingine yaani kufanikiwa kwa kimoja husaidia kufanikiwa kwa kingine, na kufanikiwa kwa vyote huleta matokeo makubwa kwa mfanya mazoezi.
Endapo mchezaji au mfanya mazoezi wa kawaida akivitekeleza vitu hivyo kwa juhudi huweza kuwa na utimamu wa mwili na hatimaye kuwa katika kiwango cha juu cha mchezo na kujenga afya bora ya mwili kiujumla.
Ili mwanamichezo aweze kucheza vizuri kwa ukakamavu huku akiwa na ustahimilivu anahitaji mlo kamili ulioandaliwa kwa kuzingatia kanuni za afya.
Wakati huo huo mlo huo huitajika kuliwa kwa ratiba maalum ambayo ikiwezekana ni ile iliyopangiwa na mtaalam wa lishe au mtaalam wa afya kama vile daktari.
Virutubisho hivi vinapatikana mwilini baada ya vyakula tunavyokula kusagwa na kuvunjwa vunjwa katika umbile linaloweza kunyonywa na seli za mwili.
Virutubisho hivi vinapatikana kwa kula vyakula vinavyotokana na mimea, wanyama na mazao ya baharini. Pia vipo vilivyotengezwa kitaalam viwandani.
Virutubisho vimeanishwa katika makundi makuu saba ikiwamo virutubisho vya wanga, mafuta, protini, vitamini, madini, nyuzi nyuzi (fibre) na maji .
Kiufupi mlo wa mfanya mazoezi unatakiwa kuwa mlo mchanganyiko huku akizingatia zaidi ulaji wa protini na mboga na matunda kwa wingi.
Mwanasoka anatakiwa kula mlo wenye kirutubisho cha protini kwa wingi kwa sababu ina kazi ya kujenga mwili ikiwamo misuli yenye majeraha, ujenzi wa kinga imara na ufanyaji kazi wa misuli kwa ufanisi.
Ni kawaida wanasoka wakimataifa kumkuta akiwa anakula mnofu wa kilo ya samaki au nyama, kuku mzima au nusu ya maharage ya soya hii ni kutokana na kuelewa vyema umuhimu wa protini mwilini.
Vile vile mwanamichezo anaweza kupewa nyongeza ya protini ya ziada iliyotengezwa kitaalam kama unga au kinywaji vinavyojulikana kama Protein supplements.
Virutubisho vya kitaalam hutumika kwasababu vyakula tunavyokula kiwango cha Protini kinaweza kisitoshe na pia kiwango cha protini hizi za ziada huingia na kufyonzwa mwilini kwa haraka
Katika kula ni lazima kuendane na unywaji maji kwani ni kitu nyeti katika shughuli zote za mwilini, tunapata maji kupitia vyakula tunavyokula na maji ya asili toka katika vyanzo mbalimbali.
Mwanamichezo anatakiwa kunywa maji mengi angalau glasi 10-20 au lita 1.5 -3 kwa siku kwani wao hupoteza maji mengi kwa njia ya jasho na kupumua wakati wa mazoezi na mechi.
Kula kuendane na udhibiti wa uzito wa mwili, mazoezi na kula vinatakiwa kuwa katika uwiano rafiki kwani ukila sana ukajipunja mazoezi inaweza kukusababishia kuwa na uzito mkubwa au unene.
Mwanamichezo hutakiwa kutumia muda mwingi kutulia na kupumzika na kulala masaa 6-8 kwa usiku mmoja ili kuupa nafasi mwili kujijenga na kujiponesha vijeraha vidogo vya ndani kwa ndani ya misuli na viungo vingine.
Kulala ni pale mwili unapokuwa hauna mawasiliano ya nje ukiwa umelala pasipo fahamu na mwili kujikita na mawasiliano ya ndani ya mwili wakati kupumzika ni mwili unakuwa macho na katika fahamu lakini viungo vinakuwa tuli pasipo kujishughulisha.
Kwa kawaida kulala huwa ni baada ya masaa mawili tangu kula mlo wa mwisho wa usiku. Itumie sababu ya kukaa ndani kipindi hiki cha corona kwa kumpumzika ukiwa ndani. Mazoezi ni jambo la mwisho vizuri kwa yule anayefanya mazoezi kwa afya kuyafanya kwa siku kwa muda wa dakika 30-60 kwa siku na katika siku tano za wiki.
Kwa yule mwenye kufanya mazoezi kama ajira inabidi kushikamana na muda na programu aliyopangiwa na wakufunzi wa mchezo unaocheza. Nidhamu ndiyo nyenzo inayomfanya mtu kuwajibika na kutekeleza maelekezo mbalimbali anayopewa.
Mfano vile vitu vyote anavyokatazwa kutumia na mtaalam wa lishe za michezo ikiwamo ulevi, matumizi ya tumbaku, anasa na ulaji holela wa vya kula mtaani ikiwamo soda, chipsi, nyama choma na vyakula vya migahawa ya magharibi na vile vya kusindika au supamaketi.
Vitu hivi vinne huzoeshwa kwa mchezaji au mwanamichezo akiwa kinda na hapo baadaye huwa ni sehemu ya maisha yake ya kila siku hivyo kumfanya kuzingatia makatazo, miiko na kuzingatia kanuni za lishe.
Nihitimishe kwa kushauri wanamichezo ambao wapo ndani kujiepusha na misongamano na mikusanyiko isiyonalazima kwa kuwa watulivu na kujikinga na kuwakinga wengine na maambukizi ya COVID-19.
No comments:
Post a Comment