
MMOJA ya wadau wa muziki waliowatoa vijana wengi kwenye fani hiyo nchini na aliyewahi kuwa Meneja wa makundi ya TMK Family na Yamoto Band, Said Fella ‘Mkubwa Fella’ amesema yeye atakuja kulipwa na mwenyezi Mungu kutokana na mchango wake anaoutoa kwa vijana.
Fella, mmoja wa vigogo wa Kituo cha Mkubwa na Wanawe ni moja ya walezi wenye uchu wa kuiona tasnia hiyo inapaa zaidi ndiye aliyewaibua Dogo Aslay, Beka Freva, Maromboso, Enock Bella, Kayumba na wasanii wengine wengi.
Akizungumza na Mwanaspoti Fella amesema baada ya kuwepo kwa majibizano katika mitandao ya kijamii na Kayumba aliyewahi kuwa mshindi wa BSS juu ya zawadi alizopewa na uhalisia wa sh mil 50 alizotangazwa kupewa.
Katika majibizano yao, Kayumba alionekana kulalamikia zawadi hiyo kuwa licha ya kupewa vitu lakini havikuendana na uhalisia wa pesa husika na ndipo Fella akamjibu kwa kutaja vitu alivyopewa ikiwemo gari pamoja na kufanya video nchini Afrika Kusini.
Fella amesema yeye katika maisha yake, atakuja kulipwa na Mungu huku akiwataka vijana wanaopitia kwake hata kama wamepata uongozi mwingine wakumbuke fadhila.
“Mimi baada ya kuona Kayumba analalamika mitandaoni kuhusu zawadi ya BSS ndipo nikasema nimkumbushe, alinunua gari na kupata kibanda, ukafanya video Sauzi alipata mpaka na mke na mtoto kupitia pesa za BSS, 2015 ni mbali yawezekana amesahau,’’ amesema Fella ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Kilungule.
Baada ya Fella kusema hayo Kayumba naye kupitia ukurasa wake wa kijamii naye alijibu ‘’Hilo gari nililonunua tulienda wote show Room au uliniletea na kadi isiyokuwa na jina langu? Na hiyo nyumba nilinunua kiwanja nikaanza kujenga au baada ya wewe kutupeleka katika nyumba ulizowajengea kaka zangu ukanionyesha msingi ambao ulianza kujenga alafu ukaniambia utamalizia.”
“Kuhusu Video Afrika Kusini ulisema Madame amejitolea kufanya yeye kama yeye kwa sababu alitaka msanii anaetoka katika shindano lake afanye vizuri katika game ya Bongo, naona hayo ndiyo unayoyahesabu katika mil 50 baba mlezi,” amesema Kayumba.
No comments:
Post a Comment