
Nairobi. Nyota wa zamani wa Manchester United, Dwight Yorke amempigia debe rafiki yake mkubwa, kocha Ole Gunnar Solskjaer kwamba atapata mafanikio katika timu hiyo.
Wawili hawa walicheza pamoja kwa miaka mingi hivyo kila mmoja ana uwelewa mzuri kuhusu uwezo wa mwenzake. Jumapili iliyopita Yorke alitua Nairobi kwa ajili ya kupigia debe Whisky ya Chivas Regal ambayo kwa sasa inashirikiana na klabu ya Manchester United kibiashara na alitumia fursa hiyo kusherehekea na mashabiki wa United usiku huo.
Ilikuwa ni siku ambayo pia Manchester United ilichuana na wabishi wao wa miaka mingi Manchester City na Yorke alipata fursa ya kucheki mchezo huo pamoja na mashabiki hao wa Manchester United katika klabu ya Disuit D2.
Yorke (48), aliwaambia wahabahari kabla ya mechi hiyo ambayo United ilishinda kwa mabao 2-0, kuwa ana imani na mwenzake huyo kwamba ndiye atakayeirejesha timu hiyo kwenye ubabe iliokuwa nayo enzi za kocha Alex Ferguson.
“Nina imani kubwa na kocha wetu, kile anachozidi kukifanya ni kitu cha kutia moyo. Anajaribu kuunda kikosi cha wachezaji wachanga matata watakaoweza kuisukuma timu mbele na kuturejesha kwenye ubabe wetu” Yorke alisema, “tuna wachezaji kadhaa wachanga tuliowasajili wanaofanya mambo hasa mchango wa Aaron Wanna Bissaka na Bruno Fernandes.”
Mzaliwa huyo wa Trinadad & Tobago kwa sasa ni balozi wa Man U na katika enzi za uchezaji wake, aliunda kombinisheni matata na straika mwenzake Andy Cole aliyeifungia United jumla ya magoli 93 kutokana na mechi 195. Ole Gunnar aliyekuwa mdogo wao mara nyingi alitumika kama super sub, akitoka benchi kujaza nafasi ya ama Cole au Yorke.
No comments:
Post a Comment