
Kocha wa timu ya Taifa ya wanawake chini ya miaka 17, Bakari Shime amesema kikosi chake kipo tayari kuivaa Uganda katika mchezo wa marudiano kuwania kufuzu Fainali za Kombe la Dunia unaofanyika leo nchini humo.
Timu hizo zinarudiana baada ya mchezo wa kwanza Tanzania kuifunga Uganda mabao 2-1 Machi Mosi kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, mabao yote mawili yakifungwa na Aisha Masaka na mshindi wa jumla wa mchezo huo atakutana na mshindi kati ya Cameroon na Sao Tome & Principle katika hatua ya pili.
Timu hiyo iliondoka jana asubuhi kwenda Uganda huku Shime akisema wamefanya maandalizi mazuri na anaamini watapata ushindi.
“Itakuwa mechi ngumu kwani tuko ugenini lakini nimekaa na vijana wangu na nimewaambia umuhimu wa mechi hiyo, hivyo naamini hawatawaangusha Watanzania,” alisema.
Kuhusu mechi hiyo, Aisha alisema, “kama kila mchezaji atajituma hakuna wa kutuzuia kupata ushindi. Naomba Mungu anisaidie niweze kufunga mabao mengi ili niisaidie timu yangu kusonga mbele na niibuke mfungaji bora wa haya mashindano.”
Aisha anaongoza kwa ufungaji bora wa mashindano hayo hadi sasa akiwa na mabao matano akifuatiwa na Blessing Kieh wa Liberia na Khaoula Knia wa Morocco wenye mabao manne kila mmoja.
Nahodha wa timu hiyo Irene Kisisa alisema wamejiandaa vya kutosha na wanajua Uganda ni timu ngumu lakini watapambana ili kuhakikihsa hawaangushi Watanzania.
No comments:
Post a Comment