
London, England. Liverpool haitapewa ubingwa wa Ligi Kuu ya England ikiwa tatizo la virusi vya corona litalazimisha msimu kumalizika kabla ya mechi zote kutimia kama ilivyothibitishwa na Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Ulaya (UEFA), Aleksander Ceferin.
Virusi vya Corona vimesababisha kusimamishwa kwa muda kwa ligi hiyo hadi Aprili 4 huku Liverpool wakiwa wanaongoza kwa tofauti ya pointi 25 lakini wataalamu wanaamini hali itazidi kuwa tete zaidi siku za usoni jambo linaloleta wasiwasi kama msimu unaweza kumalizika au vinginevyo.
Kumekuwa na fikra na mitazamo mingi juu ya kumaliza ligi pasipo kucheza mechi zisizosalia ambapo kuna wanaotaka Liverpool ipewe ubingwa kwa vile inaongoza na wengine wanashauri msimu ufikie tamati bila kuwa na bingwa, lakini Ceferin ameondoa uwezekano wa Liverpool kupewa kombe hilo.
“Nimeona na nimesikia habari feki kuwa Uefa itashauri ligi imalizike na timu iliyo nafasi ya kwanza ndio itangazwe mabingwa. Ninaweza kusema sio kweli. Lengo letu ni kumaliza ligi na hatushauri jambo lolote kama hilo kufanyika katika chama chochote au ligi.
Kauli ya Ceferin imetolewa katika kipindi ambacho ligi mbalimbali zimegoma kutumia njia ya kuipa ubingwa timu inayoongoza msimamo wa ligi na badala yake zimeamua kusubiri kwa muda ili kuona kama tatizo hilo litapungua ziweze kuendelea.
Miongoni mwao ni ile ya Ligi Kuu Hispania ‘La Liga’ ambayo haiwezi kuikabidhi Barcelona ya Nou Camp ubingwa kabla haijakamilisha idadi ya mechi zote msimu huu.
No comments:
Post a Comment