
Dar es Salaam. Endapo atashinda pambano la Machi 21 nchini Ujerumani, bondia Hassan Mwakinyo ataandika historia mpya.
Bondia huyo ana historia katika ngumi baada ya ile ya mwaka 2018 aliyoiweka England alipomchapa Samm Eggington.
Mwakinyo bondia namba moja nchini uzani wa super welter atamkabili Jack Culcay katika mji wa Bayerhalle, Wuppertal, Nordrhein-Westfalen.
Mwaka 2018 Mwakinyo alimchapa Eggington kwa Technical Knock Out (TKO) raundi ya pili katika pambano lililokuwa la raundi 10.
Pambano hilo lilimpandisha Mwakinyo katika viwango vya ubora na kuwa bondia wa 19 duniani kabla ya kupanda hadi nafasi ya 17 lakini hivi karibuni aliporomoka hadi nafasi ya 20.
“Akishinda Ujerumani itakuwa nafasi nzuri kwake kwani bondia anayepigana naye si mwepesi,” alisema kocha Abdallah Salehe aliyekuwa akimnoa Francis Cheka.
Mpinzani wa Mwakinyo ambaye ni bondia wa nyota nne na nusu anashika namba 14 kwenye viwango vya dunia vinavyojumuisha mabondia 1855 akimuacha Mwakinyo ambaye ni bondia wa 20 kwenye uzani wa super welter kwa nafasi sita.
Katika mapambano sita ya mwisho Mwakinyo alishinda yote na mpinzani wake matano na kupigwa.
Bondia huyo (34) anatumia mkono wa kulia (orthodox) sawa na Mwakinyo ambaye ana miaka 25 ingawa anazidiwa uzoefu ulingoni na mpinzani wake.
No comments:
Post a Comment