
Mwanza. Kocha wa Coastal Union, Juma Mgunda amesema licha ya kupata pointi tatu dhidi ya Singida United, lakini haikuwa rahisi kutokana na upinzani waliopata katika mchezo huo.
Coastal Union ikiwa ugenini juzi mkoani Singida, iliichapa Singida United bao 1-0 na kuifanya timu hiyo kuendelea kubaki mkiani kwa pointi 12 na kuongeza presha ya timu zenye hatari ya kushuka daraja msimu ujao. Akizungumza jana, Mgunda alisema walishuka uwanjani kusaka ushindi ili kufuta maumivu kutokana na kupoteza mchezo baina yao na Mwadui, jambo ambalo walifanikiwa licha ya upinzani waliopata dhidi ya Singida.
Alisema wachezaji walipambana na kufuata maelekezo ya benchi la ufundi na malengo yao yalitimia huku akibainisha kuwa kwa sasa hakuna mchezo rahisi katika mashindano hayo.
“Tunashukuru kwa alama tatu, lakini haikuwa mechi rahisi wapinzani walihitaji ushindi ukizingatia hawako nafasi nzuri vijana wangu walipambana na kupata bao ambalo limetupa pointi tatu,” alisema kocha huyo.
Kocha huyo ambaye ni nyota wa zamani wa Taifa Stars, alisema kuwa zipo kasoro ambazo zilionekana katika mchezo huo na mkakati wake ni kupata matokeo mazuri katika kila mchezo ili kujiweka katika mazingira bora.
No comments:
Post a Comment