Search This Blog

Wednesday, March 4, 2020

RC Tabora ataka majinaya vigogo wanaofanya biashara haramu


MKUU wa Mkoa wa Tabora, Aggrey Mwanri, amemtaka Mrajisi Msaidizi wa Ushirika wa mkoa huo kupeleka ofisini kwake majina ya watumishi na viongozi wanajihusisha na biashara haramu ya mazao ya biashara, ili hatua za kisheria zichukuliwe dhidi yao.


Alitoa agizo hilo wakati wa Kikao cha Ushauri cha Mkoa (RCC) cha kupitia mapendekezo ya bajeti ya mwaka ujao wa fedha.

Alisema vitendo hivyo ni tatizo kwa wakulima na vinawafanya waendelee kuwa maskini na halmashauri za wilaya kupata mapato kidogo ya ushuru wa mazao.

Mwanri alisema haiwezekani kila wakati Ofisi ya Mrajisi Msaidizi inatoa taarifa kuwa kuna baadhi ya viongozi wa serikali, wa kisiasa na vyama vya ushirika wamejiingiza kwenye biashara ya vishada na uuzaji wa pembejeo bila kuwataja majina.

Alisema serikali kupitia Waziri Mkuu ilishatoa maelekezo kuwa mtu akayeruhusiwa kuuza tumbaku ni yule ambaye ana shamba la tumbaku na zao hilo litauzwa kupitia ushirika.

Kamati hiyo iliviomba vyombo vya ulinzi na usalama, ikiwamo Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kuchunguza na kuwafuatilia wanaojihusisha na vitendo hivyo ili wachukuliwe hatua za kisheria.

Ilisema vitendo hivyo ni kosa kutokana na wahusika kutoa rushwa na udanganyifu kwa ajili ya kumnyonya mkulima na kuibia serikali mapato yake yanatokana na ushuru wa mazao.

Katibu Tawala Mkoa wa Tabora, Msalika Makungu, alisema kuna baadhi ya viongozi wanashiriki katika biashara chafu ya uuzaji na ukopeshaji wa fedha kwa wakulima kwa riba kubwa na kuwafanya kuendelea kuwa maskini.

Alisema kuna baadhi ya wakulima wamekuwa wakikopeshwa pembejeo na fedha kwa mara mbili ya bei halali kwa madai kuwa pindi watakapovuna tumbaku, ni lazima wampe sehemu ya tumbaku kama malipo ya deni.

Makungu alisema vitendo hivyo vimefanya wakulima wengi wakati wa kuuza tumbaku yao kubaki na fedha kidogo na sehemu kubwa ya mauzo inaenda kwenye deni.

No comments:

Post a Comment

Punguza kilo tano kwa siku saba

  NI watu wachache wanaopenda kunenepa, wengi wanapenda miili ya wastani kwa kuwa  unene si mzuri. Ukiwa mnene si tu kwamba unakaribisha m...